DSC_0002
Mkurugenzi Mkazi wa ASASI isiyo ya kiserikali ya kupiga vita umaskini Actionaid Tanzania (AATZ), Yaekob Metena akifungua kongamano la siku tatu kwa asasi zisizo za kiserikali, wawakilishi kutoka makundi ya vijana na waandishi wa habari juu ya masuala ya haki kwenye kodi linaloendelea kwenye hoteli ya Seascape jijini Dar.(Picha na Zainul Mzige wa MOblog)

Na Mwandishi wetu
MAMLAKA mbalimbali ambazo zinawajibika kwa namna moja au nyingine katika kuwezesha mizigo mbalimbali inayoingia nchini kutolewa bandarini zitaunganishwa na mfumo mpya wa kisasa wa kutumia mtandao wa kompyuta wa Tanzania Customer Integrated System (TANCIS) kwa lengo la kuharakisha uondoaji wa mizigo hiyo.
Kauli hiyo imetolewa na Meneja wa elimu kwa walipa kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Diana Masalla wakati akitoa mada katika kongamano lililoandaliwa na asasi isiyo ya kiserikali inayoendeshwa bila faida ikiwa na lengo la kupiga vita umaskini Actionaid Tanzania (AATZ) ikishirikiana na Kikundi cha haki kwenye kodi (Tanzania Tax justice Group).
Kongamano hilo ambalo linahusu haki kwenye kodi ni sehemu ya mpango wa asasi ya Action Aid Tanzania kuleta uelewa na weledi katika masuala ya kodi miongoni mwa watanzania na walipa kodi ili kufanikisha ukusanyaji wa raslimali zinazowezesha serikali kutoa huduma za msingi na pia kutengeneza fursa za wananchi kujiendesha kiuchumi.
Masalla alisema mfumo huo mpya ambao utamfanya mwenye mzigo kutoa maelezo ya mzigo wake kidigitali na maofisa forodha nao kushughulika na mzigo wake bila kukutana naye ana kwa ana, umeonesha ufanisi mkubwa hasa wa ufuatiliaji wa hatua kwa hatua tangu mzigo umeingia nchini hadi unamfikia mhusika.
Aidha mfumo huo umebana uchepushaji wa mizigo hiyo kutokana na ufuatiliaji wa kidigitali unaofanywa na mfumo huo.
DSC_0008
Meneja uratibu na mahusiano wa Action Aid Tanzania Bibi Jovina Nawenzake akielezea historia fupi ya ActionAid Tanzania na kazi wanazozifanya.
Alisema ingawa kumekuwepo na kilio kikubwa cha ucheleweshaji wa mizigo na kusukumiwa lawama hizo TRA, lakini kiukweli kuna mambo ambayo yanaingiliana na mamlaka zingine na mzigo hauwezi kutolewa mpaka mamlaka hizo ziseme na kwa mfumo wa zamani ilikuwa inachukua muda kuhangaika ofisi moja hadi nyingine.
Alisema mathalani kwa bidhaa za pembejeo , dawa na mazao mengine yenye sheria za kimataifa, mizigo yake haiwezi kuingia mpaka TBS au TFDA au wizara husika iidhinishe.
Alisema kuundwa kwa mamlaka na taasisi hizo katika mfumo mpya kutasaidia kila kitu kwenda kigitali na hivyo kuharakisha kasi ya uondoaji mizigo bandarini kutokana na kuongezeka kwa kasi ya utoaji wa vibali na ulipaji wa kodi.
Akiwasilisha mada ya uelewa wa misingi ya kodi na uchambuzi wa misingi ya sera ya kodi nchini Tanzania, Masalla alisema kwamba mfumo huo pamoja na kunung’unikiwa Julai mwaka huu baada ya kuzinduliwa Oktoba mwaka jana, maboresho makubwa yamefanyika ili kuufanya ujibu mahitaji ya wananchi na walipa kodi.
Miongoni mwa maboresho hayo ni kuweka kompyuta takribani 20 katika chama cha mawakala wa utoaji mizigo nchini TAFFA ambapo zinatumiwa na watumishi wa TRA kuingiza takwimu na kusaidia kujibu hoja za watumishi wa TRA kwa njia za mfumo wa kompyuta.
DSC_0116
Meneja wa elimu kwa walipa kodi kutoka mamlaka ya mapato Tanzania (TRA), Diana Masalla, akiwasilisha mada ya uelewa wa misingi ya kodi na uchambuzi wa misingi ya sera ya kodi nchini wakati wa kongamano hilo.
Masalla alisema kwamba mfumo mpya unaleta makampuni na mamlaka zote husika katika mwavuli mmoja na hivyo kurahisisha utoaji huduma na kudhibiti upotevu wa mapato ya serikali.
Akifungua kongamano hilo Mkurugenzi mkazi wa Action Aid Yaekob Metena alisema kwamba ni lengo lao kuhakikisha kwamba kila mtanzania anajua misingi ya kodi na kwamba bila kodi serikali haiwezi kufanya majukumu yake ya msingi kama ukusanyaji wa rasilimali kwa ajili ya kuzitumia katika kazi nyingine.
Alisema kutokana na kukosekana kwa haki katika kodi kumefanya serikali kupoteza fedha nyingi ambazo zingeliweza kutumika kwa ajili ya kufungua fursa za ajira na pia kuhudumia shughuli za afya.
Mkurugenzi huyo alisema lengo kuu la kongamano hilo kutambua misingi ya kodi na sababu zake na pia kuelewa kwamba kuna haki ya kodi ambayo inamtaka kila mwananchi na mfanyakazi iwe wa umma au watu binafsi kutambua ushiriki wake katika kuiwezesha serikali kuwa na makusanyo makubwa ya kodi kwa maendeleo ya taifa.
Metena alisema: kama hakuna uelewa wa haki ya kodi na wahusika nao wakasababisha kodi isikatwe serikali itakuwa inapoteza fedha nyingi.
“Kama hakuna haki katika kodi, serikali haitaweza kukusanya mahitaji yake ambayo yanasubiriwa na watu wake”
DSC_0004
Pichani juu na chini ni baadhi ya washiriki wanaohudhuria kongamano la haki kwenye kodi lililoandaliwa na shirika la Actionaid Tanzania.
Amesema mfumo wa kodi unaposhindwa kuwafanya watu wote kushiriki katika kuitendea haki serikali kwa kulipa kodi ambayo ndiyo msingi wa mapato yanayochangia maendeleo na ustawi wa jamii.
Kongamano hilo la Actionaid Tanzania linafanyika katika hoteli ya Seascape iliyopo jijini Dare s salaam, lengo kuu likiwa kuhamasisha watu kutambua misingi ya kodi, sababu na serikali yenye makusanyo mazuri ya kodi inavyoweza kutengeneza fursa nyingi za kiuchumi ili wananchi wake waweze kuzitumia.
Lengo la kongamano hilo ikiwa kutanua uelewa na weledi wa washiriki ambao wengi wao ni kutoka asasi zisizo za kiserikali na waandishi wa habari wanaotakiwa kujua masuala ya kodi, baada ya mada mbalimbali, ofisa wa TRA aliulizwa kuhusu misamaha ya kodi.
DSC_0128
Katika kongamano hilo pia waandishi wa walijifunza utendaji wa serikali na pamoja na kuitaka serikali kuhakikisha kwamba wadau wenye fedha wanaotoa michango yao kwa ajili ya bajeti ya taifa na kuboresha huduma za msingi kwa wakati kwa Tanzania.
Aidha washiriki wengi katika kongamano hilo walihoji kisa cha serikali kung’ang’ania Pay as you earn (PAYE) kwa wafanyakazi na kuacha vyanzo vingine huku misamaha ya kodi ikiendelea kuitafuna.
Wakati huo huo katika mazungumzo na waandishi wa habari Masalla amewataka waandishi wa habari/jamii kufichua wakwepa kodi.
Aidha alisema kwamba sheria mpya ya VAT itaondoa misamaha mingi na hivyo kuisaidia serikali.
Pia amesisitiza wateja wanapofanya manunuzi kudai risiti.
DSC_0135
Mkufunzi wa kongamano la siku tatu la haki kwenye kodi, Bwana Mosses Kulaba kutoka kituo cha uendeshaji uchumi na sera za biashara, akiwasilisha mada inayohusu mfumo wa kodi nchini Tanzania na changamoto zake katika ukusanyaji kodi.
DSC_0099
Mmoja wa washiriki katika semina hiyo aliyeibua hoja ya kuwepo kwa jitihada za makusudi kwa mamlaka ya mapato Tanzania (TRA), kujikita katika kutafuta vyanzo vipya vya mapato kuliko kujikita katika kodi zilizozoeleka kama PAYE inayolenga kukusanya kodi zaidi kutoka kwa wafanyakazi na wafanyabiashara wadogo wadogo.
DSC_0088
Ndugu Anwar Mkama mwakilishi kutoka vyombo vya habari akiuliza swali kwa meneja elimu kwa walipa kodi juu ya changamoto za mfumo wa kodi nchini ni namna gani wanazishughulikia ili kuboresha ukusanyaji wa mapato na kupunguza urasimu.