Bwana David Nabarro
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa anayehusika na ugonjwa wa Ebola David Nabarro ameiambia BBC kuwa mlipuko wa ugonjwa huo magharibi mwa Afrika unaweza kudhibitiwa katika kipindi cha miezi mitatu.
Dr.Nabarro alisema kuwa ina maana kuwa VISA vipya vya ugonjwa huo vitapungua kila wiki.
Amesema kuwa kwa sasa maambukizi ya ugonjwa wa Ebola ni ya juu hata baada ya kuwepo kwa jitihada za kimataifa.
Nabarro amesema kuwa kuuelewa ugonjwa wa Ebola miongoni mwa jamii zilizoathirika kutasaidia kupambana nao kwa kuwa watu wanaelewa kwamba kuwatenga wagonjwa ndiyo njia bora ya kuzuia maambukizi.
Zaidi ya watu 4000 wameaga dunia kutokana na ugonjwa wa Ebola wengi kutoka mataifa ya Sierra Leone, Liberia na Guinea.