UNESCO-logo1
SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limesema hakuna makubaliano yaliyofikiwa kati yake na mamlaka husika nchini Tanzania za kuwezeshwa kujengwa kwa bwawa la kufua umeme la Stiegler’s Gorge .
Ofisi za Shirika hilo zilizopo jijini Dar es salaam mwishoni mwa wiki wametoa taarifa ya kukanusha maelezo yaliyoandikwa na gazeti la The Guardian (ref:http://www.ippmedia.com/frontend/index.php?l=72984) kwamba yapo maafikiano kuhusu ujenzi wa bwawa hilo.
Eneo la Stiegler’s Gorge lipo katika hifadhi ya Selou ambayo ni sehemu ya urithi wa kimataifa ambapo ujenzi wa miundombinu yoyote yenye athari kubwa katika hifadhi hiyo lazima kuwepo na maridhiano kati yake na mamlaka husika.
Taarifa hiyo imesema taarifa zilizoandikwa na gazeti hilo Oktoba 8, mwaka huu limeshutua shirika hilo. Taarifa hizo zilizokuwa ukurasa wa mbele zilisema kwamba Tanzania itavuna zaidi nishati ya umeme kutokana na maafikiano yake na UNESCO juu ya ujenzi wa wa bwawa hilo.
Katika taarifa yake UNESCO imesema kwamba katika mkutano wa 36 wa kamati ya Urithi wa dunia (WHC) uliofanyika Saint-Petersburg mwaka 2012 na ule wa 37 uliofanyika Phnom Penh, mwaka 2013 na wa mwisho uliofanyika Doha mwaka huu ulieleza wazi mashaka yake juu ya athari ya ujenzi wa bwawa hilo katika hifadhi.
Katika mikutano yote hiyo ilikubalika kwamba mamlaka zinaozohusika nchini kutofanya shughuli zozote za maendeleo ndani na kwenye mipaka ya hifadhi bila kupata kibali cha WHC kwa mujibu wa kifungu 172 cha makubaliano.
Aidha kamati hiyo iliitaka mamlaka zinazohusika kutekeleza ushauri uliotolewa na kamati ya pamoja kati ya WHC na Muungano wa ushirikiano wa hifadhi ya asili (IUCN) wa kutengenezwa kwa mkakati kabambe wa menejimenti ya Ekolojia ya Selous.
Aidha inatakiwa kutayarisha menejimenti hiyo kwa kuweka mipaka katika eneo la urithi wa dunia na kuonesha maeneo ambayo yanastahili kuingizwa katika hifadhi.
Pia kufafanua mradi wa Stiegler's Gorge, hatua iliyofikiwa hasa katika maamuzi na kuhakikisha kwamba ufahamu kuhusu athari, gharama, manufaa na namna inavyofaa au kutofaa na pia kuwa na mpango mbadala kama haikuwezekana.
Mambo yote hayo yanatakiwa kuzingatia umuhimu wa eneo hilo kwa jamii ya dunia na hivyo kuangalia vigezo vyote vya maeneo ya urithi .
Katika maamuzi hayo pia Kamati ya Urithi ilifurahishwa na nia ya mamlaka husika za Tanzania kuendesha utafiti huo kwa mujibu wa makabaliano na vigezo stahiki ili kuelewa athari zake katika hifadhi hiyo ambayo ni urithi wa kimataifa, korido za mapito ya wanyama na nini kitatokea kwa korido la Selous-Niassa Corridor.
Kwa mujibu wa taarifa ya UNESCO, kamati hiyo ya Urithi wa Dunia (WHC) ilitarajia kupata taarifa za awali Februari Mosi mwakani.
Aidha taarifa hiyo ilitakiwa kuwa na muhtasari wa hatua mbalimbali zinazchukuliwa na muda wake kuhusiana na hifadhi ya Selou kujiondoa katika urithi wa dunia ulio katika hatari ya kutoweka.
Imeelezwa kuwa taarifa hiyo ndiyo itakuwa msingi wa majadiliano katika mkutano ujao wa WHC wa 39 utakaofanyika Bonn Ujerumani.
Aidha taarifa hiyo imesema kutokana na vitu vyote kutokuwa bado kufanyika msimamo wa UNESCO unabaki kama ulivyo, kwamba hakuna makubaliano yoyote yaliyofikiwa na kinyume na hapo ni kukiuka makubaliano.