Uraia katika Jamhuri ya muungano wa Tanzania kutoka katika Rasimu ya katiba inayopendekezwa
Uraia wa Jamhuri yaMuungano
65.-(1) Mtu ambaye, kabla ya Katiba hii kuanza kutumika, ni raia wa
Jamhuri ya Muungano ataendelea kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano.
(2) Uraia wa Jamhuri ya Muungano ni wa aina mbili na utapatikana kwa
njia ya kuzaliwa au kuandikishwa.
Haki ya uraia 66. Kila raia ana haki ya kutambuliwa uraia wake na kwa
madhumuni haya, mamlaka ya nchi itaweka utaratibu wa sheria
utakaowezesha raia kupata hati ya kuzaliwa, kitambulisho cha uraia wake bila ya
upendeleo na ubaguzi wa aina yoyote, na pale inapohitajika, nyaraka za
kumwezesha kusafiri.
Uraia wa kuzaliwa
67.-(1) Kila mtu aliyezaliwa Tanzania Bara au Zanzibar atakuwa raia wa
kuzaliwa wa Jamhuri ya Muungano iwapo, wakati wa kuzaliwa, mama au baba
yake ni, au alikuwa raia wa Jamhuri ya Muungano.
(2) Kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii, mtu aliyezaliwa nje ya
Tanzania atakuwa ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa kuzaliwa kuanzia
tarehe ya kuzaliwa kwake ikiwa mama au baba yake ni raia wa Jamhuri ya
Muungano.
(3) Endapo mmoja kati ya wazazi wake alifariki kabla ya mtu
huyo kuzaliwa, uraia wa mzazi huyo wakati wa kifo chake unatumika, kwa
madhumuni ya kutambua uraia wa mtu huyo aliyezaliwa baada ya mzazi
aliyefariki kana kwamba mzazi huyo alikuwa anaishi hadi kuzaliwa kwa mtu
huyo.
(4) Mtoto mwenye umri chini ya miaka saba akikutwa ndani ya eneo
la Jamhuri ya Muungano katika mazingira ambayo wazazi wake
hawajulikani, atachukuliwa kuwa ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa
kuzaliwa.
(5) Endapo uraia wa wazazi wa mtoto aliyepewa uraia chini ya
masharti ya ibara ndogo ya (4) utabainika kuwa si uraia wa Jamhuri ya
Muungano, uraia wa mtoto huyo utasita.
(6) Bila kuathiri masharti ya Ibara hii, Bunge litatunga sheria ambayo
itaweka masharti na utaratibu wa:
(a) upatikanaji wa uraia kwa watu waliozaliwa na raia wa Tanzania nje
ya nchi;
(b) kurudisha uraia wa watu ambao uraia wao ulifutwa baada ya kupata
uraia wa nchi nyingine; na
(c) mambo mengine ambayo yatatakiwa kutungiwa sheria.
Uraia wakuandikishwa
68.-(1) Mara baada ya kuanza kutumika kwa Katiba hii, mtu
ambaye amekuwa mkaazi wa Jamhuri ya Muungano na ambaye ametimiza
masharti yote ya sheria za nchi anaweza kuomba kuandikishwa kuwa raia wa
Jamhuri ya Muungano.
(2) Mtu aliyefunga ndoa na raia wa Jamhuri ya Muungano na
ambaye:
(a) amedumu katika ndoa hiyo kwa kipindi cha miaka saba
mfululizo; na
(b) ametimiza masharti yaliyoainishwa katika sheria kwa mujibu wa
ibara ndogo ya (1),
anaweza kuomba uraia wa kuandikishwa kuwa raia wa Jamhuri ya
Muungano.
(3) Endapo ndoa iliyotajwa katika ibara ndogo ya (2) itavunjika,
kama mtu huyo hakuukana uraia wake wa Tanzania, ataendelea kuwa raia wa
Jamhuri ya Muungano.
(4) Mtoto aliyezaliwa katika ndoa iliyorejewa katika ibara ndogo ya (2),
atakuwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa kuzaliwa.
(5) Mtoto aliye na umri wa chini ya miaka kumi na nane ambaye
wazazi wake si raia wa Tanzania, akiasiliwa na raia wa Jamhuri ya
Muungano, kuasiliwa kwake, kutawezesha mtoto huyo kuwa raia wa Jamhuri
ya Muungano wa kuandikishwa.
(6) Bunge litatunga sheria, pamoja na mambo mengine, kusimamia
masuala yanayohusu uraia wa Jamhuri ya Muungano.
Hadhi maalum ya watu wenye asili au nasaba ya Tanzania
69. Bila kuathiri masharti yaliyomo kwenye Sura hii, mtu yeyote
mwenye asili au nasaba ya Tanzania na ambaye ameacha kuwa raia wa Jamhuri
ya Muungano kwa kupata uraia wa nchi nyingine, atakapokuwa katika Jamhuri
ya Muungano, atakuwa na hadhi maalum kama itakavyoainishwa katika sheria
za nchi.
0 Comments