Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe akifafanua jambo. Picha na Maktaba
Dodoma/Arusha. Serikali za China na Tanzania, zimetoa matamshi makali dhidi ya kile zilichokiita “taarifa za uongozi na uzushi” ambazo zinahusisha ndege ya Rais wa China, Xi Jinping na usafirishaji wa vipande vya meno ya tembo kutoka Tanzania.
Jana kwa nyakati tofauti, Balozi wa China hapa nchini, Lu Youqing, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu walitoa taarifa wakituhumu taasisi iliyotoa ripoti hiyo kwamba malengo yake ni kuharibu uhusiano mwema baina ya nchi hizo.
Ripoti ya taasisi ya Uingereza iitwayo Environmental Investigation Agency – EIA (Wakala wa Uchunguzi wa Mazingira) iliyotolewa juzi, inawatuhumu maofisa na wanausalama waliokuwa katika msafara wa Rais Jinping wakati wa ziara yake nchini Tanzania Machi 2013, kwamba walitumia fursa ya kidiplomasia kusafirisha vipande vya meno ya tembo katika ndege ya rais.
Hata hivyo, Balozi Youqing aliliambia gazeti hili mjini Arusha kuwa taarifa hizo zimetolewa na watu wasiopenda maendeleo ya nchi maskini na kuongeza: “Ni uongo, uongo mkubwa, kama angejitokeza hadharani mtu kama huyo anastahili kuadhibiwa vikali na mwongo ni lazima aadhibiwe.”
“Taarifa hizi za uongo na zisizo na chembe ya ushahidi zimetolewa na watu wasiopenda maendeleo ya nchi maskini kama Tanzania,” alisema Balozi Youqing baada ya ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Kuzuia Ujangili unaoendelea jijini Arusha.
Alisema tuhuma hizo zimetolewa na watu wasio na ushahidi na kwamba lengo lake ni kuharibu jina na sifa ya taifa lake mbele ya jumuiya ya kimataifa.
Kauli bungeni
Mjini Dodoma Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alitoa kauli ya Serikali bungeni akisema tuhuma dhidi ya msafara wa Rais Jinping hazina ukweli wowote na kwamba hata madai kuwa serikali haijali wala haichukui hatua dhidi ya wanaojihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo siyo za kweli.
“Taarifa za taasisi ya EIA ni za kupikwa na kuungwaungwa ili kuchafua heshima ya nchi yetu, pamoja na kuchafua heshima ya rafiki zetu wa China,” alisema Membe na kuongeza: “Ni taarifa iliyoandaliwa na kutolewa wakati huu kukidhi ajenda mahususi ambayo tunaifahamu fika.”
Membe alisema mtoa taarifa ambaye ametajwa kuwa chanzo cha habari ni mtu mmoja ambaye walimkuta barabarani na kuanza kumuuliza maswali wakati mtu huyo siyo mtumishi wa bandari wala uwanja wa ndege.
“Ni mpitanjia tu wa mitaani. Hata video ya mahojiano inaonyesha hivyo,”alisema Membe.
Kwa upande wake, Waziri Nyalandu alisema uhusiano wa Tanzania na China ni wa muda mrefu na kuheshimika kiasi kwamba taarifa hizo zimeisononesha serikali. “Tunakamata Wachina wengi sana kwa tuhuma za kukutwa na meno ya tembo, lakini hii ya ndege ya Rais ni matusi,”alisema.Ukaguzi wa ndege
Nyalandu alisema ni kweli kwamba Wachina wamekuwa wakihusishwa na biashara ya meno ya tembo na wamekamatwa wengi, lakini kuhusisha ndege ya Rais wa China ni uongo kwani ndege hizo hukaguliwa na maofisa usalama wa pande zote.
Balozi Youqing akizungumzia suala hilo alisema Tanzania imefanya kazi nzuri katika kupambana na ujangili na kwamba inasikitisha kusikia inahusishwa na masuala ambayo si ya ukweli, kwani hata msafara wa viongozi wa nchi hizo hukaguliwa kabla ya safari.
“Mimi ndiye niliyeratibu safari nzima wakati wa ziara ya Rais, hivyo ningejua kinachotokea, kwani hata mimi mwenyewe nilikuwa nakaguliwa na maofisa wa usalama wa China na wa Tanzania, isingewezekana,” alisema Balozi Youqing.
Ziara ya Jinping
Akizungumzia zaidi ziara ya Rais Jinping, Membe alisema ilikuwa ya saa 24 na programu yake ilianza mara tu alipowasili nchini na kutokana na ratiba ilivyokuwa kwa rais na wajumbe wake isingewezekana ununuzi wa aina yoyote kufanywa na ujumbe huo.
“Alianza na dhifa ya kitaifa, akaenda kuzindua ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere, akawa na mkutano na Rais wa Zanzibar pia na Rais Mstaafu Benjamin Mkapa baada ya hapo walikwenda kwenye makaburi ya Wachina kule Majohe na kisha kuondoka kwenda uwanja wa ndege. Sasa hizo ‘shopping’ zilifanyika saa ngapi?” alihoji Membe.
Alisema ni muhimu kujiuliza kwa nini taarifa hizo zitoke leo hasa baada ya ziara ya Rais Jakaya Kikwete nchini China na kwa nini ije baada ya Rais kuhutubia mafanikio ya ziara hiyo.
“Jibu kila mmoja anaweza kujua. Wasambazaji wa taarifa hizi hawaitakii mema nchi yetu. Hawawatakii mema marafiki zetu wa China. Wamejawa na wivu na husuda kwa mafanikio ya China na inashangaza kuona wanawachukia huku wanawategemea,” alisema Membe.
Kauli yake inaungwa mkono na ile ya Nyalandu ambaye alisema:
“Rais wa China alikuwa katika ziara ya pili tangu aingie madarakani baada ya kwenda Urusi na akaja Tanzania ambako alitoa mwelekeo wa serikali yake katika uhusiano wa nchi yake na Afrika”.
Alisema hii ni mara ya pili kwa vyombo vya habari vya nje kutoa taarifa mbaya kuhusu Tanzania kabla ya kuanza kwa mikutano mikubwa kimataifa kuhusiana na majangili, akirejea habari zilizoandikwa na Daily Mail la Uingereza siku moja kabla ya Rais Kikwete kuhudhuria mkutano nchini Uingereza.“Leo wamejua kutakuwa na mkutano mkubwa kama huu na masikio ya watu yakielekezwa Arusha ndiyo habari hii inatoka.”
Mkutano wa Arusha
Awali akizungumza katika mkutano wa kutokomeza ujangili, Balozi Youqing aliitaka serikali ya Tanzania kuanza kutoa adhabu kali kwa watu wanaojihusisha na ujangili.
Alisema nchini China wanaokutwa na hatia ya makosa kama hayo adhabu yao huwa ni kunyongwa hadi kufa.
Balozi huyo alisema Serikali yake imekuwa ikitoa misaada ya fedha na utaalamu katika kukabiliana na ujangili nchini Tanzania na kuwa mafanikio yameanza kuonekana.
Naye Nyalandu alisema Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine kimataifa imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kutokomeza ujangili.
“Matokeo makubwa yamepatikana na katika kipindi kifupi, kwani kwa miezi minne sasa Tanzania inaweza kujivuna, kwani hakuna tembo hata mmoja aliyeripotiwa kuuawa katika pori la akiba la Selous,” alisema Waziri Nyalandu.
Mkutano huo wa kikanda unajadili mbinu za kupambana na ujangili na utoroshwaji wanyama katika nchi za ukanda wa Bahari ya Hindi, Afrika Mashariki na Sudan Kusini.