Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamadi akizungumza jambo.

KUNA mambo mengi ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambayo yamekuwa yakiutesa. Lakini Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamadi aliiambia Tume ya Warioba iliyokuwa ikishughulikia rasimu ya katiba mambo hayo.

Kwa faida ya wasomaji wetu, leo tunawadonolea kwani anatuletea kumbukumbu za miaka ya nyuma sana ‘makengeza’ ya muungano ambayo yanasumbua hadi sasa.
Katika makubaliano ya kimataifa yaliyounda Muungano Aprili 24, 1964 (wa Tanganyika na Zanzibar), ambayo hata hivyo, katika muda wote wa uhai wa muungano yamekuwa hayafuatwi, hakuna kifungu hata kimoja kilichotoa au kuagiza kwamba Serikali ya Tanganyika ifutwe kwa mujibu wa makubaliano hayo.


Serikali ya Tanganyika, kama ilivyo ile ya Zanzibar, imelindwa na kifungu cha (v) kinachosomeka hivi: “The existing laws of Tanganyika and of Zanzibar shall remain in force in their respective territories…”. Kinachosemwa hapa ni kwamba: “Sheria zilizopo za Tanganyika na za Zanzibar zitaendelea kufanya kazi na kuwa na nguvu katika maeneo yao.”

Wataalamu wa katiba na sheria wanafahamu kwamba katiba ndiyo sheria mama ya sheria zote za nchi. Hivyo Katiba ya Tanganyika imelindwa na inapaswa kuwepo na serikali yake iwepo, pamoja na viongozi wake kuwepo na kusimamia mambo yasiyo ya Muungano.

Katiba na sheria za Tanganyika ndizo zilizotakiwa zitumike katika eneo la Tanganyika kwa yale mambo yaliyokuwa hayamo kwenye muungano kama ambavyo Katiba (au kabla ya hapo Dikrii za Kikatiba – Constitutional Decrees) na sheria za Zanzibar zinavyotumika katika eneo la Zanzibar kwa yale mambo ambayo si ya Muungano.

Hiyo ndiyo tafsiri ya ‘maeneo yao’.
Wazanzibari wanafahamu kwamba Katiba na Serikali ya Tanganyika vimefutwa kwa makusudi na Bunge la Tanganyika ili kujipa nafasi kuitumia Serikali ya Muungano, kama kwamba ndiyo Serikali ya Tanganyika. Lengo ni hatimaye kuiua Serikali ya Zanzibar na kufanya Tanganyika mpya ikiwa na jina jipya la Tanzania lenye mipaka mipya, yaani kuwa nchi moja yenye serikali moja.

Kwa kusaidia, ni vyema ikaangaliwa Sheria Na. 22 ya mwaka 1964 inayoitwa “Union of Tanganyika and Zanzibar Act, 1964.”

Sheria hii ilipitishwa na Bunge la Tanganyika Aprili 25, 1964, siku moja kabla Muungano kuanza kufanya kazi. Ilikusudiwa kuthibitisha kukubalika muungano huo wa Tanganyika na Zanzibar upande wa Tanganyika (ratification). Kifungu cha (viii) cha Makubaliano ya Muungano kinaagiza ifanyike hivyo kwa pande zote mbili za Muungano.

Inasikitisha kusoma katika kifungu Na. 2 cha sheria hiyo kwamba:
“Existing law” means the written and unwritten law as it exists immediately before Union Day … but does not include the Constitution of Tanganyika insofar as it provides for the Government of the Republic of Tanganyika or any declaration or law, or any provision thereof, which expires with effect from commencement of the Interim Constitution”. (“Sheria iliyopo maana yake ni sheria iliyoandikwa na isiyoandikwa kama ilivyo kabla tu ya siku ya Muungano…

lakini haijumuishi Katiba ya Tanganyika kwa mintarafu ya kuiweka kwake Serikali ya Jamhuri ya Tanganyika au tamko au sheria, au kifungu chochote ambacho kinafutika kwa kuanza kufanya kazi Katiba ya Muda (ya Muungano).”

Kwa hivyo, wakati Bunge la Tanganyika linapitisha sheria ya kuridhia (ratify) kuwepo kwa Muungano kwa upande wa Tanganyika, sheria hiyo ilianza kupinga vifungu vya makubaliano hayo.

Itaendelea wiki ijayo.