Stori: Mwandishi Wetu
HALI tete! Bado vuguvugu la madai ya kuvunjika kwa ndoa ya mtangazaji mahiri Bongo, Gardner Gabriel Fikirini Habash ‘Kapteni’ na Mbongo Fleva, Judith Daines Wambura Mbibo ‘Lady Jaydee au Jide’, sasa lingine limeibuka ambapo mali za wawili hao zinatajwa kuzua utata, Risasi Jumamosi linachambua.Kwa mujibu wa chanzo cha ndani, Gardner ameshapeleka hati ya kesi kwa mwanasheria wake kwa kusudio la kumpandisha kizimbani mtalaka wake huyo ili mgawo wa mali ujulikane na kila mmoja apate haki yake.
KILICHOZINGATIWA
Kilichozingatiwa katika mgawo huo ni uhalali wa ndoa yao iliyofungwa Mei 14, 2005 ambapo mali zote zilizopatikana ndani ya ndoa ni za wote kwa mujibu wa sheria ya Ndoa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.“Gardner anataka mgawo wake, lakini sasa utata ulioibuka ni kwamba, inaonekana kama mali zote ni za Jide kwa vile zimeandikwa majina yake hivyo jamaa ana wasiwasi kwamba Jide anaweza kusema mahakamani kuwa alizichuma mali hizo kabla ya ndoa,” kilisema chanzo hicho kilicho jirani na familia hiyo.
Chanzo hicho kiliendelea kudai kwamba, utata huo umemfanya Gardner kuwa bize ili kuhakikisha anaumaliza hususan kwenye nyumba yao iliyopo Mbezi ambapo wengi wanaamini ilijengwa kwa kutumia fedha ya Jide kabla hawajafunga ndoa.
MALI ZINAZOTAJWA
Mali zinazotajwa kuibua utata ni Mgahawa wa Nyumbani Lounge uliopo Kinondoni, Dar ambao hivi karibuni Jide aliubadili jina na kuuita M.O.G Restaurant. Mgahawa huo walipangishwa na mtu Kuna madai kwamba, Jide na Gardner kabla ya ndoa yao kuparaganyika walikwenda kwa mmiliki huyo na kusema wameamua kuuacha baada ya mkataba wao kumalizika. Lakini kilichoonekana baadaye, Jide alirudi kwa njia ya uani na kuanzisha mkataba mpya bila Gardner na kuuita M.O.G.
Mali nyingine mbali na nyumba na mgahawa ni mabasi madogo mawili aina ya Toyota Hiace, moja la Machozi Band na la M.O.G Restaurant. Mabasi hayo yameandikwa Lady Jaydee & Machozi Band. Hata hivyo, yapo madai kwamba Machozi Band nayo imebadilishwa jina, sasa inaitwa Lady Jaydee & The Band.
Mali nyingine ni Albamu zote za Jide alizotoa tangu mwaka 2005 wakiwa tayari kwenye ndoa ambapo kwa kawaida mauzo yake ni endelevu na gari la kutembelea aina ya Range Rover Vogue.
Albamu hizo ni Moto (2005), Shukrani, The Best of Lady Jaydee (2006) na Nothing But the Truth (2014).KAMA NI KUPATA
Chanzo kinabainisha kuwa, uhakika wa mali anazoweza kupata Gardner ni mgawo wa pesa kwa mauzo ya gari hilo la kutembelea na nyumba ambapo inaaminika ndiyo mali ya kifamilia zaidi.
SHERIA YA TALAKA
Risasi Jumamosi lilitembea ofisi za Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (Rita) jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujua sheria za talaka zinasemaje!
1. Mwenza mwenye nia ya kuomba ndoa ivunjwe anatakiwa kupeleka malalamiko yake Baraza la Usuluhishi la Ndoa linalotambuliwa kisheria ambapo ni Ofisi ya Kamishna wa Ustawi wa Jamii, Baraza la Kata, Mabaraza ya Ndoa ya Kidini katika Misikiti
na Makanisa.
2. Baraza litasikiliza malalamiko na likishindwa kusuluhisha, hati maalumu itaandikwa kwenda mahakamani ikielezea mgogoro kwa kifupi na baraza kutoa maoni yake kwa suala husika.
4. Mahakama itasikiliza shauri husika na ikiridhia itatoa tamko la kuvunjika kwa ndoa (decree).Tamko la kuvunjika ndoa litawasilishwa Rita kwa ajili ya kusajiliwa na kuingizwa katika daftari la talaka. Baada ya hapo msajili atatoa hati ya talaka ambayo ni uthibitisho wa kuvunjika kwa ndoa na utaratibu wa mgawanyo wa mali utafuata kwa kila kilichochumwa (hata kijiko) wakati watalaka hao wakiwa ndani ya ndoa.
JIDE AFICHA MAWASILIANO YAKE
Risasi Jumamosi lilimsaka Jide kwa njia mbalimbali lakini hakupatikana. Baadhi ya watu wamesema kwa sasa mwanamuziki huyo ameficha mawasiliano yake.ALICHOSEMA GARDNER
Gardner alipotafutwa na mwandishi wetu kwanza alianza kwa kukana madai kwa mtindo huu.
Mwandishi: (anajitambulisha kwa jina na kampuni anayofanyia kazi), najua uko kwenye mgogoro wa mali na shemeji (Jide).
Gardner: Kwanza huo mgogoro unaniambia wewe, mimi siujui. Lakini kwa hayo unayotaka kuniuliza nasema no comment (sina cha kusema).
0 Comments