Waziri Kiongozi Mstaafu wa awamu ya sita, Shamsi Vuai Nahodha.
Waziri Kiongozi Mstaafu wa awamu ya sita, Shamsi Vuai Nahodha amesema ipo haja ya kuendelea na Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa vile sababu zilizofanya kuundwa kwake baada ya vyama vya CCM na CUF kuunda serikali hiyo bado zipo.
Katika mahojiano haya maalum kati ya kiongozi huyo na gazeti hili yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar, Nahodha amezungumzia mengi kuhusu katiba mpya, Ukawa, serikali ya kitaifa, kujiuzulu kwake uwaziri, asichoweza kukisahahu katika uongozi wake kama Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), uchumi na kadhalika. Ungana nami ufahamu alichokisema:

Mwandishi: Unaweza kuwaambia wasomaji historia yako kifupi?
Nahodha: Mimi nilizaliwa Novemba 20, 1962 Makunduchi Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja na kupata elimu yangu katika Skuli ya Msingi Kiongoni huko Makunduchi na kuendelea Sekondari katika Skuli ya Benbella na kisha kufanikiwa kujiunga katika Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni. Shahada ya kwanza niliipata Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika fani ya elimu na pia stashahada niliyoipata katika Chuo cha Diplomasia, Dar.
Mwandishi: Kisiasa, umewahi kushika yadhifa zipi nchini?
Nahodha: Mwaka 2000 nikiwa na umri wa miaka 38 nilikabidhiwa cheo cha juu kabisa katika nchi ya Zanzibar kwa kuteuliwa na Rais wa wakati huo, Aman Abeid Karume kuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Nilijishangaa kwa kuteuliwa lakini niliyapokea maamuzi ya rais kwa mikono miwili na kuingia kazini katika Ofisi ya Waziri Kiongozi Vuga, Zanzibar.
Kisiasa niliwahi pia kuwa Mwakilishi wa wananchi (Mbunge) wa Mwera mwaka 2000 hadi 2005 kisha Mwanakwerekwe 2005 hadi 2010. Niliwahi kuingia katika kinyan’ganyiro cha kugombea urais mwaka 2010 ambapo jina langu  lilivuka Kisiwandui na kuweza kufika Dodoma lakini kwa bahati mbaya halikurudi.
Kabla ya hapo nilikuwa mwakilishi na mwaka huo niligombea tena uwakilishi  na kushinda kwa kishindo. Baadaye nikateuliwa kuwa Mbunge na Rais Jakaya Mrisho Kikwete katika Serikali ya Muungano  kisha nikawemo katika baraza la mawaziri wa Muungano baada ya kupewa wadhifa wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi baadaye nikahamishiwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Mwandishi: Ukiwa waziri kiongozi ulishuhudia ushindani wa hali ya juu wa kisiasa katika visiwa hivyo, unazungumziaje hilo hasa uchaguzi wa mwaka 1995? Nahodha: Matokeo ya chaguzi kuu tangu mwaka 1995 yameonyesha hakuna tofauti kubwa ya ushindi kati ya CCM na CUF, pamoja na kuwa katika chaguzi zote 1995, 2000, 2005 na 2010 CCM ilishinda lakini tofauti ya mshindi na mpinzani wake haikuwa kubwa sana.
Ingawa CCM kiliendelea kushinda kwa asilimia 51, 52, na 54, hali hiyo inaonyesha kuwa chama cha upinzani CUF pia kina nafasi kubwa tu ya kushinda kwa sababu hupigiwa kura na takriban nusu ya Wazanzibari.
Mwandishi: Kutokana na ushindi kukaribiana, nini maoni yako?
Nahodha: Iko haja ya kutambua kuwa ushindani huu unahitaji kuangaliwa kwa umakini mkubwa kwa vile wataalamu wa mambo ya siasa wanasema mahali kwenye ushindani wa nguvu msipokuwa na utaratibu mzuri wa kugawana madaraka, hapatakuwa na utulivu utakaosaidia kuwaletea maendeleo wananchi mnaokusudia kuwaongoza.
Itaendelea Jumanne ijayo.