Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.PICHA|MAKTABA
Arusha. 
Jumuiya ya kimataifa imepitisha Azimio la Arusha lenye lengo la kukabiliana na ujangili na kuendeleza wanyama.
Azimio hilo limepitishwa baada ya mkutano wa siku mbili ambapo pia imekubalika kwamba hali ya baadaye ya wanyama barani Afrika ni suala linalohitaji uwajibikaji wa pamoja.
Aidha, nchi za Afrika zimetakiwa kuukomesha ujangili na kufanya juhudi ya kuhakikisha wanyama walio katika hatari ya kutoweka wanalindwa na kuhakikisha kundi hilo linakua.
Wanyama ambao kwa sasa wapo hatarini kutoweka ni tembo, faru na simba.
Mkutano huo uliojumuisha mataifa mbalimbali ya Afrika na jumuiya za kimataifa na kufunguliwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete, umetoa wito kwa mataifa yote kufanya kazi kwa pamoja kukabili ujangili kwa kushirikisha wananchi wanaoishi na kutegemea wanyamapori hao na mapori yenyewe.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mtaalamu wa Mawasiliano wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, Hoyce Temu, baada ya mkutano ambao uliangalia sheria zilizopo za kulinda mapori na wanyamapori, uhalisia wa mifumo ya ujangili na uhifadhi, washirika wa maendeleo nao walielezea nia zao za kuendelea kusaidia uhifadhi wa wanyamapori na mapori katika ukanda wa Afrika ikiwamo Tanzania.
Awali akifungua mkutano kwa niaba ya Rais Kikwete, Waziri Nyalandu alisema kwamba mataifa yasidharau nguvu ya pamoja katika kukabiliana na ujangili.
Alisema kwamba hali ya baadaye ya wanyamapori katika bara la Afrika ni wajibu wa kila mtu na kila taifa na mamlaka nyingine ambazo ni wadau.
Alisema Tanzania katika mchango wake imeanzisha mkakati wa kukabiliana na ujangili na kuunda mamlaka ya wanyamapori ili kuwa na uhakika wa kuendeleza masuala yanayohusu hifadhi na changamoto zake kwa kasi na karibu zaidi.
Akizungumza kwa niaba ya ICCF ambao ni wenyeji wenza wa mkutano huo, Makamu Mwenyekiti Dk Kaush Arha, alisema mkutano huo ulikuwa na manufaa makubwa hasa wito wa kuweka mikakati ya kurejesha makundi ya wanyama walio katika hatari ya kutoweka.
Naye Mkuu wa balozi za nchi za Jumuiya ya Ulaya nchini, Balozi Filiberto Ceriani Sebregondi ameipongeza Tanzania kwa hatua iliyochukua kukabiliana na ujangili.