Tume ya Ulaya imepitisha hatua za kujilinda katika kujaribu kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa mafua ya ndege baada baada ya matukio mapya ya ugonjwa huu kuripotiwa nchini Uingereza na Uholanzi.
Hatua hizo ni pamoja na kuwaua wanyama walio katika maeneo yaliyoathirika kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa mafua ya ndege na kupiga marufuku uuzaji wa bidhaa za ndege kutoka maeneo hayo.Serikali ya Uholanzi imeripoti maumbukizi ya kirusi hatari aina ya H5N8 katika shamba moja la ndege nchini humo.

Uingereza imeripoti mlipuko wa mafua ya ndege huko Yorkshire Mashariki, na tume imesema milipuko hiyo "huenda ikafanana".Kirusi aina ya H5N8 kinaweza kuambukiza binadamu.
Maafisa wa Umoja wa Ulaya wamesema milipuko hii huenda ikahusiana na mafua ya ndege iliyoripotiwa nchini Ujerumani hivi karibuni.
Wanasema inawezekana ugonjwa huu umesambazwa na ndege pori wanaohama hama wakielekea kusini majira ya baridi kali, lakini matukio hayo yanaendelea kuthibitisha uhusiano uliopo kati ya matukio matatu yaliyoripotiwa.
Tume ya Ulaya imesema katika taarifa yake kuwa Uingereza na Uholanzi tayari wanatekeleza maelekezo katika kuwaondoa ndege walioathirika, kuzuia mauzo ya bidhaa za ndege walioathirika na ndege hai na kuanzisha ukanda wa kuzuia maambukizi.
Taarifa imesema: "Lengo la hatua hizi ni kudhibiti ugonjwa huu na kuzuia kusambaa kwa virusi hatari vya mafua ya ndege katika nchi zilizoathirika na kwenye nchi nyingine na nchi nje ya hapo."