Temeke ni moja kati ya wilaya tatu zinazounda Jiji la Dar es Salaam. Pia ni jimbo la uchaguzi linaloongozwa na Mheshimiwa Abbas Mtemvu kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM).Temeke inapatikana Kusini mwa Jiji la Dar es Salaam ambapo kwa upande wa Mashariki, kuna Bahari ya Hindi, Kusini inapakana na Wilaya ya Mkuranga na Kaskazini na Magharibi inapakana na Wilaya ya Ilala.Wiki iliyopita, Uwazi lilisaga lami hadi katika jimbo hilo na kutembelea kata mbalimbali zikiwemo Mbagala, Mbagala Kuu, Chamazi, Tandika, Temeke, Keko, Chang’ombe, Azimio, Yombo Vituka na nyingine nyingi ambapo lilizungumza na wananchi mbalimbali walioeleza kero zinazowasumbua.
MATATIZO YA WANANCHI
Mwanahamisi Matiku, mkazi wa Keko Magurumbasi, alikuwa na haya ya kusema: “Jamani huku kwetu Keko utafikiri hakuna serikali. Biashara ya uchangudoa imeshamiri sana Keko Machungwa, Keko Magurumbasi, Toroli na maeneo mengine. Yaani ngono inafanyika hadharani huku watoto wetu wakiona na kondomu zinatupwa hovyo mitaani. Tunaomba mbunge atusaidie kwani imekuwa ni kero.”
Jibu: Mbunge hakupokea simu mara zote alizopigiwa. Hata alipotumiwa ujumbe, hakujibu.
Ismail Lyandele mkazi wa Temeke Mwisho, yeye alikuwa akihitaji ufafanuzi kutoka kwa mbunge:
“Mheshimiwa mbunge wetu. Wakati wa kampeni zako, uliahidi kututatulia kero ya maji inayotutesa kwa kipindi kirefu. Wake zetu wanalazimika kuamka alfajiri sana kusaka maji na kuhatarisha usalama wao. Je, ahadi yako imefikia wapi? Mbona bado maji ni tatizo Temeke?”
Jibu: Mbunge hakupokea simu mara zote alizopigiwa. Hata alipotumiwa ujumbe, hakujibu.
Isihaka Mwakibete, mkazi wa Chamazi yeye alitaka ufafanuzi kutoka kwa mbunge wake kuhusu ubovu wa barabara ya kutoka Mbagala kuelekea Chamazi na maeneo mengine.
“Barabara imejaa mashimo na sehemu nyingine hakuna lami kabisa utafikiri hatuishi Dar es Salaam, yaani sehemu ya kusafiri kwa dakika kumi mtu unakaa hata saa nzima njiani. Mbunge kazi yake nini? Anasubiri uchaguzi ukaribie aje kutoa ahadi nyingine wakati za mwanzo bado hajazitimiza.Jibu: Mbunge hakupokea simu mara zote alizopigiwa. Hata alipotumiwa ujumbe, hakujibu.
“Tatizo letu sisi wananchi wa hapa Mtoni kwa Aziz Ali ni uchafu uliokithiri, angalia mifereji imeziba, chemba za maji machafu zinafumuka hovyo na mvua ikinyesha kidogo tu basi hakukaliki, watu wanatapisha vyoo bila utaratibu.
Yaani tunaishi kwa miujiza tu, afya zetu na watoto wetu zipo mashakani, utafikiri hatuna mbunge bwana! Angalia kila sehemu mitaani kuna madampo yasiyo rasmi, watu wanamwaga takataka hovyo,” alisema Uledi Mtima, mkazi wa Mtoni kwa Aziz Ali jijini Dar es Salaam.
Jibu: Mbunge hakupokea simu mara zote alizopigiwa. Hata alipotumiwa ujumbe, hakujibu.
“Jamani Temeke tunaishi utafikiri wakimbizi, giza likishaanza kuingia tu mitaani hakukaliki kutokana na vibaka na wakabaji. Yaani mtu unapigwa roba hadharani na hakuna wa kukusaidia, unaporwa na kupigwa utafikiri hakuna polisi. Tunamuomba mbunge wetu atusaidie,” alisema Hussein Ngulwa.
Matatizo mengine yaliyoainishwa na wananchi wa Temeke, ni pamoja na shida ya usafiri kwa wananchi wa maeneo ya Mbagala ambapo hulazimika kugombea magari kutoka sehemu mbalimbali za jiji kuelekea makwao kutokana na wingi wa abiria na uhaba wa magari.
Huduma za kijamii pia ni tatizo lingine lililobainishwa likiwemo uhaba wa dawa na uwezo mdogo wa Hospitali ya Wilaya ya Temeke kuwahudumia wananchi wote wa jimbo hilo na matatizo mengine lukuki. Uwazi lilipojaribu kumtafuta Mbunge Mtemvu, simu yake ya mkononi ilikuwa ikiita bila kupokelewa, hata alipotumiwa ujumbe hakujibu mpaka tunaenda mitamboni.