Baadhi ya Wahitimu wa Chuo cha Maendeleo ya Utalii Zanzibar wakiingia katika Viwanja vya Mahafali chuoni hapo.
Mgeni Rasmi katika Mahafali ya Sita ya Chuo cha Maendeleo ya Utalii Zanzibar Waziri wa Fedha wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Saada Mkuya akitoa hotuba kwa wahitimu hawapo pichani ambapo amewataka wajiajiri wenyewe badala ya kutegemea Serikali.
Baadhi ya Wahitimu wa Fani ya Upishi wakiwa wanamsikiliza Mgeni Rasmi Waziri wa Fedha wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Saada Mkuya hayupo pichani wakati wa sherehe ya Mahafali ya Sita ya Chuoni hapo.
Baadhi ya Wahitimu wa Fani ya Ukarimu na Uongozi wa Hoteli wakivaa kofia kuashiria kukabidhiwa Stashahada zao katika Mahafali ya sita ya Chuo cha Maendeleo ya Utalii Zanzibar.

Mwanafunzi Bora Chuoni hapo wa Fani ya Mapokezi ya Wageni “Front Office”Said Shaame Khamis akipokea Zawadi kutoka kwa Mgeni Rasmi Waziri wa fedha wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Saada Mkuya katika Mahafali hayo Yaliyofanyika Maruhubi mjini Zanzibar.
Mgeni Rasmi Waziri wa Fedha wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Saada Mkuya katikati mwenye miwani akiwa katika Picha ya pamoja na viongozi wa chuo na Wahitimu wa mahafali ya sita ya Chuo cha Maendeleo ya Utalii Zanzibar. (Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar).
Waziri wa Fedha wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Saada Mkuya amewataka Wahitimu wa Chuo cha Maendeleo ya Utalii Zanzibar kutoitegemea Serikali katika kupata ajira badala yake wajikite katika kujiajiri wenyewe.
Amesema nafasi za Ajira Serikalini ni chache hivyo Wahitimu hao wanapaswa kujishughulisha ili wajiajiri wenyewe au kupitia Taasisi Binafsi.
Waziri Mkuya ameyasema hayo alipokuwa akitoa hutuba yake kwa Wahitimu wa Mahafali ya Sita ya Chuo cha Maendeleo ya Utalii yaliyofanyika leo kati viwanja vya Chuo hicho Maruhubi Mjini Zanzibar.
Amesema dhana ya kuitegemea Serikali katika ajira kwa sasa haina nafasi kutokana na uchache wa Ajira na kwamba anaamini Elimu waliyoipata Wahitimu inaweza kuwasaidia katika kujiajiri.
Ametoa Rai kwa Wahitimu hao kujiunga na Kampuni za Ulinzi ambazo zinatarajiwa kuanzishwa Zanzibar kutokana na kuripotiwa kwa matukio mbalimbali ya kihalifu nchini.
Aidha Waziri Mkuya amewashauri Wahitimu hao kutotosheka na kiwango cha Elimu walichofikia badala yake wajiendeleze mbele ili kupata ufanisi katika kazi zao.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Chuo hicho Bi Zulekha Khamis Omar amesema Chuo hicho kinazidi kupiga hatua kimaendeleo nakwamba Wanatarajia kuanzisha Masomo ya Shahada ya Kwanza mwaka 2017-18.
Amesema mipango ipo mbioni kukamilika kuhusu kuanzishwa kwa Masomo ya Shahada ambapo Chuo hicho kitakuwa Chini ya Chuo Kikuu cha Zanzibar SUZA.Hata hivyo Bi Zulekha alizitaja Changamoto zinazokabili Chuo hicho kuwa ni pamoja na Uhaba wa Vifaa katika Jiko, na Mmommonyoko wa Ardhi unaotishia Mazingira ya Chuo hicho.
Chuo hicho kilichoanzishwa mwaka 1992 ili kuongeza ukuaji na Maendeleo ya Utalii Zanzibar kimefanya Mahafali yake ya sita ambapo Jumla ya Wahitimu 511 wa Ngazi za Stashahada na Cheti katika Fani mbalimbali wamehitimu.