Sengerema ni moja kati ya wilaya saba zinazounda Mkoa wa Mwanza. Upande wa Kaskazini na Mashariki imezungukwa na Ziwa Victoria, upande wa Kusini kuna Mkoa wa Geita na Kusini Mashariki kuna Wilaya ya Misungwi.
MATATIZO YA WANANCHI
Licha ya kuwa jimbo hilo lipo pembezoni mwa Ziwa Victoria, uhaba wa maji ni kero kubwa inayowatesa wananchi wa Sengerema, kiasi cha kuathiri sana shughuli za maendeleo.
Tunatembea umbali mrefu sana kufuata maji, kwa mfano sisi hapa maji tunachota kwenye Bwawa la Mzungu, ni mbali sana isitoshe maji yenyewe, ngombe wanakunywa hayohayo, watu wanaoga humohumo na sisi tunachota ya kwenda kupikia na kunywa, tunaishi utafikiri hakuna serikali, tunaomba mheshimiwa mbunge atusaidie, alisema Innocent Maguha, mkazi wa jimbo hilo.
Matatizo mengine yaliyoelezwa na wananchi ni ukosefu wa vyoo, ofisi za walimu na upungufu wa madawati katika shule nyingi za msingi za jimbo hilo.
Wanafunzi wengi wakitaka kujisaidia wanaenda vichakani au ziwani, jambo ambalo ni hatari sana kiafya, tunaomba serikali ilitazame hili kwa upana, alisema Swebe Matiku, mkazi wa jimbo hilo.
Tatizo lingine lililopo katika shule za msingi ni utoro wa wanafunzi, watoto wa kiume wanaacha kusoma na kwenda kufanya kazi za uvuvi ziwani huku watoto wa kike nao wakirubuniwa na wavuvi na kujikuta wakiishia kupata mimba, Omary Seif aliliambia Uwazi.
Mabere Steven, yeye aliibua kero nyingine kuwa ni ukosefu wa huduma bora za afya kwa wananchi wa jimbo hilo.
Yaani kama huna pesa ukiumwa unaweza kufa kwani ukienda hospitali hata kama una bima ya afya utaambiwa madawa hakuna ukajinunulie kwenye maduka binafsi, alisema. Tatizo lingine ni ubovu wa miundombinu ikiwemo barabara kwenye jimbo hilo.
Kero nyingine tunatozwa fedha nyingi wakati wa kuandikisha watoto kuanza shule, kila mtoto anatakiwa kulipiwa shilingi elfu 25 hadi 30, sasa mimi nashangaa, serikali inasema elimu ni bure mbona tunachangishwa? Tunamuomba mbunge atusaidie.
Tatizo lingine lililoelezwa na wananchi ni malalamiko kuwa polisi wanatumia nafasi yao kuwatesa wananchi kwa kuwapiga bila makosa na kuwapora mali zao hasa nyakati za usiku.
MAELEZO YA MBUNGE
Baada ya kusikia kero za wananchi, Uwazi lilianza jitihada za kumtafuta Mheshimiwa Ngeleja ambapo mwandishi wetu alifika ofisini kwake mara kadhaa na kumkosa kwa maelezo kwamba alikuwa akishughulikia tatizo la maji jimboni kwake.
Uwazi halikuishia hapo, lilijaribu kumpigia simu yake ya mkononi ambapo hakuwa akipatikana kwenye namba zote anazotumia siku zote. Uwazi linaendelea kumtafuta Mheshimiwa Ngeleja ili atoe majibu ya kero zinazowakabili wananchi wa jimbo lake.
0 Comments