STORI: Mwandishi Wetu/Amani

IMEBAINIKA! Mapambano na wahalifu wanaosadikiwa ni magaidi kwenye Kitongoji cha Amboni jijini Tanga, yameingia sura nyingine baada ya wakazi wa kitongoji hicho kuvujisha siri tano, Amani limenyetishiwa.

Polisi wakiwa kwenye mapigano na wahalifu hao.
WALIKUWA NA WAPENZI
Kwa mujibu wa mkazi mmoja wa eneo hilo, wahalifu hao walishakuwa na wanawake kwenye eneo hilo, hivyo kama walikuwa na mpango wa kujua siri za Jiji la Tanga ilikuwa rahisi sana.“Wale watu baadhi yao walikuwa na wanawake hapa Amboni. Na hilo limebainika baada ya kutokea kwa mapambano na wao kukimbia kwani na mmoja wao aliyekuwa na mwanamke hapa hajaonekana tena,” alisema mtoa habari huyo.
WALIKUWA WAKICHENJI DOLA KILA BAADA YA SIKU MBILI
Habari kutoka kwa mkazi mwingine zilidai kuwa, baadhi ya wahalifu hao walikuwa wakienda mjini Tanga kila mara kwa shida ya kuchenji dola za Kimarekani.“Kuna wakati nilikutana na watu wakisema wanatafuta maduka ya kuchenji  dola za Marekani, wakakosa na kwenda mjini. Nikawa nawaona mara kwa mara tena wakienda mjini, nadhani ni kila baada ya siku mbili.
“Lakini sikujua wanapoishi wala kazi zao. Naamini ni haohao maana baada ya mapambano na wao sijawaona tena tangu Ijumaa iliyopita,” alisema mkazi huyo aliyejitambulisha kwa jina la Hans.
TABIA ZAO
Mjumbe wa nyumba kumi wa kitongoji hicho, Idd Suleiman akizungumza na Amani alisema kuwa, kulikuwa na watu walioonesha dalili kwamba si wenyeji wa eneo la Amboni.“Mbaya zaidi, watu hawa walikuwa na tabia ya kuonekana nyakati za usiku, kama ni mchana basi si kwa uwazi mkubwa. Nilijaribu kuwafuatilia nikidhani ni wakazi wa mtaani kwangu lakini sikuwahi kuwajua,” alisema mjumbe huyo.
Paul Chagonja.
WENGI WAO NI WAREFU, WEMBAMBA, WEUSI
Mjumbe huyo alizidi kusema kuwa, watu hao waliokuwa wakionekana maeneo hayo ni wembamba, wengine ni warefu na weusi lakini walionekana wakakamavu muda wote.
“Kusema kweli kama sisi wananchi tungekuwa watafiti sana na kutoa taarifa polisi labda wangekamatwa mapema kwani watu hao walikuwa hawafanani na sisi wakazi wa eneo hili ambao tunajuana,” alisema.
NI KWELI WAMEKIMBILIA KENYA?
Naye mzee Juma Kabari ‘Mapipa’ yeye alisema kuwa, anavyojua miaka ya nyuma kuna Mzungu aliwahi kumpoteza mbwa wake ndani ya mapango hayo.“Sasa katika kumtafuta hakumpata, baadaye akaja kuonekana Mombasa nchini Kenya. Ikagundulika kuwa, kuna pango moja ambalo linatokea Mombasa. Nina wasiwasi kwamba, hata hawa jamaa (wahalifu), huenda walipita chini kwa chini wametokea Mombasa, ndiyo maana hawajawakamata.
“Watu waliodaiwa kukamatwa juzi, siamini kama kweli ni miongoni mwa wale ambao walitoa upinzani kwa askari wetu Ijumaa iliyopita,” alisema mzee Mapipa.