Wahamiaji haramu kutoka Ethiopia waliofikishwa mbele ya mahakama Kenya
Raia wa Ethiopia 100 wamekamatwa nchini Kenya katika mitaa ya mji mkuu Nairobi wakielekea Afrika Kusini.
Polisi wanasema kuwa walipitia Kenya kinyume cha sheria wakitumia mabasi tofauti lakini wakakamatwa wakipumzika katika makazi fulani viungani mwa jiji.
Wanatarajiwa kufikishwa mahakamani hapo Kesho.

Ni wakimbizi hao walipoletwa hii leo katika mahakama ya Makadara kufunguliwa mashtaka ya kuwa nchii kinyume cha sheria hali kadhalika bila vibali.
Walifika mahakamani wengi wao wakiwa wachovu kutokana na safari ndefu kutoka Ethiopia na kwa kukosa chakula.
Mmoja wao alikuwa taabani hadi hakimu akasema apelekwe hospitalini ama apewe chakula.
Wengine walinong’ona kuwa wanahisi njaa.
Hata hivyo walipoulizwa ikiwa wanaweza kuzungumza Kingereza walikana japo wakakiri kuwa wanakielwa tu kiamariki lugha asilia ya Ethiopia.
Kutokana na hali hiyo hakimu aliagiza warejeshwe korokoroni kisha wafikishwe Mahakamani hapo Kesho atakapopatikana mkalimani anayeelewa lugha yao.
Wahamiaji haramu kutoka Ethiopia waliofikishwa mbele ya mahakama Kenya
Kwa mujibu wa polisi washukiwa hao walikuwa safarini kuelekea Afrika Kusini japo walipata ugumu wa kujieleza zaidi kutokana na matatizo ya lugha.
Hii si mara ya kwanza raia wa kigeni kupatikana Kenya wakiwa safarini kuelekea mataifa mengine kujitafutia ajira ama kuwa wahamiaji katika nchi wanazodhania kuwa zitawafaa kwa ajira na maslahi mbalimbali.
Kadhalika kuna dhana kuwa wengine hutumiwa na wafanyibiashara wanaolangua watu.
Mwaka wa 2012 raia wa Ethiopia 42 walipatikana wamefariki katika lori lilokuwa limefunikwa kila mhali kwa kukosa hewa.
Ilisemekana kuwa raia hao vile vile walikuwa wakielekea Afrika Kusini mojawepo ya nchi ambazo ziajulikana kwa kuwa na wahamiaji wengi.