Na Imelda Mtema/Risasi
Mambo Vipi mpenzi msomaji wa Mpaka Home? Binafsi niko ngangari, bado nazidi kukata mbuga ili kuweza kufika katika kila nyumba ya staa hapa Bongo ili kuweza kukujuza wewe mpenzi msomaji wangu maisha halisi wanayoishi mastaa wetu na pengine kuweza kujifunza kupitia wao.

Rashid Mwishehe ‘Kingwendu’ akiwa na familia yake.
Wiki hii nilikuwa maeneo ya Kingugi- Mbagala jijini Dar, nyumbani anapoishi msanii mahiri wa vichekesho nchini, Rashid Mwishehe ‘Kingwendu’ ambapo nyumbani kwake anaishi yeye, mkewe pamoja na watoto wake watano.Ni mengi sana tumezungumza naye, tujiunge naye hapa chini:

Kwa nini umeamua kukaa mbali  na wasanii wenzako?
“Nimeamua kukaa mbali kwanza kwa sababu ni kwangu na kitu kingine sipati bugudha yoyote huku maana mastaa wengi wanapenda kujirundika sehemu moja, ukienda Sinza wamejazana, Kinondoni ndiyo usiseme sasa huku kwingine wakae akina nani? Huku napata raha duniani.”
Akicheza na watoto wake.
Maisha magumu kwa sasa, vipi kuhusu uangalizi wa watoto watano?
“Unajua siku zote Mungu ni mwema ana sababu zake maana yeye ndiyo alinipa watoto watano kwa nini sasa asinipe riziki ya kuwahudumia  watoto wangu? Hakuna hata mmoja ambaye haendi shule wala kukosa kula chakula japokuwa kweli maisha ni magumu na hawa watasoma mpaka wachoke wenyewe.”
Nini unapenda kufanya ukiwa nyumbani?
“Nikiwa nyumbani siwi kama mwanaume, namsaidia mke wangu kazi zote ikiwepo kupika na kufanya kazi  za nyumbani na wakati mwingine naenda kumsaidia biashara zake hata kumenya viazi na kuchota maji pia.”
...Akitoka kuchota maji.
Vitu gani ambavyo unavitamani nyumbani kwako havipo?
“Mwenzenu hapa kwangu natamani sana marumaru (Tiles), niweke hata madirisha ya vioo lakini naamini nitafanya tu kwa maana huko nyuma nilianza kidogokidogo mpaka nimefanikiwa na mimi napenda kweli nipendezeshe nyumba yangu ionekane vizuri kama mastaa wengine”

Unapendelea kula chakula gani?
“Sichagui chochote, mimi ni Mzaramo. Kukiwa na vidagaa sawa, bagia, ubwabwa maharage nakula wala siyo wa chipsi kuku na mayai.”Unapata muda wa kuwa na familia yako?
“Mwingi tu kwa sababu si unajua kazi hizi tumejiajiri wenyewe kwa hiyo mtu unaweza kutenga muda kabisa na mke na watoto kwa ajili ya kupanga mambo ya kifamilia zaidi.

Kingwendu akitoka kuchuma mboga 'Kisamvu'.
Sanaa yake pekee ndiyo inakuendeshea maisha yako?
“Haa wapi? Sanaa hii ya vichekesho siyo kabisa hapa kinachonisaidia zaidi ni vibiashara ambavyo mke wangu anafanya ndiyo angalau maisha yanaendelea lakini sanaa peke yake ingekuwa shida kubwa sana jamani.”
Kuna ishu ilizagaa ulitengana na mkeo, ni kweli?
“Mbona hiyo zamani jamani na nilishasahau kabisa mimi sasa hivi tuko shwari na imara tunalea watoto wetu kwa raha zetu na maisha yanaendelea huku mapenzi yakizidi kuongezeka maana watoto watano siyo mchezo.”