Andrew Carlos/Risasi
IKIWA imebaki wiki na siku kadhaa kufika Aprili 5, mwaka huu (Sikukuu ya Pasaka) ambapo ndani ya Uwanja wa Taifa wa Burudani, Dar Live uliopo Mbagala-Zakhem, jijini Dar kutakuwa na bonge moja la shoo kutoka kwa Ali Kiba ‘Mwana Dar Live’ kizuri ni kwamba atakayefunika kwa kucheza Wimbo wa Chekecha Cheketua kuzawadiwa.

Ali kiba.
Akizungumza na Mikito Nusunusu, mratibu wa burudani katika ukumbi huo, Abdallah Mrisho ‘Abby Cool’ alisema kuwa mbali na uwepo wa Mwana Dar Live siku hiyo pia ataandika historia ya aina yake.

“Wote tunajua kuwa Wimbo wa Chekecha Cheketua ndiyo wimbo wa mjini kwa sasa. Niwaambie tu kitu kizuri ni kwamba kutakuwa na mashindano ya kuucheza wimbo huo na atakayefunika siku hiyo tutampa zawadi nono,” alisema Abby.
SHOO YA KIHISTORIA
Abby aliongeza kuwa mara ya mwisho kwa Mwana Dar Live kufanya shoo ya kufa mtu ilikuwa ni mwaka 2013 ambapo kipindi hicho aliwapagawisha mashabiki kwa ngoma zake kali zisizochuja kama Dushelele, My Everything, Single Boy na nyingine nyingi.
“Mwana Dar Live amerudi upya kufanya shoo ya kihistoria na kipindi hiki amerudi akiwa na ngoma mpya kabisa zinazotikisa kila kona ya dunia kama Mwana, Kimasomaso pamoja na Chekecha Cheketua.
“Mashabiki wajiandae kwa sapraizi kibao kutoka kwake ikiwa ni pamoja na kuwaonjesha ngoma zinazobamba alizofanya na mdogo wake wakiwa kama Kiba Square ambazo ni Kidela, Pita Mbele na nyingine nyingi.”
ISHA MASHAUZI KUFUNIKA
Mbali na Mwana Dar Live pia kwa wale mashabiki wa muziki wa Pwani watakata kiu na kundi zima linalosumbua kwa sasa la Mashauzi Classic chini ya Malkia wa Masauti, Isha Mashauzi.
“Isha amekuwa na vionjo vya aina yake katika suala zima la kuimba na amekuwa akiwavutia mashabiki wengi kwa kuchanganya muziki huo na vionjo vya Bongo Fleva na vigodoro.”
“Miongoni mwa nyimbo zitakazosumbua siku hiyo ni Ropokeni Yanawahusu iliyoimbwa na Saida Ramadhan, Ni Mapenzi tu ya Zubeda Malik pamoja na wimbo ambao ni habari nyingine kwa sasa ujulikanao kama Bonge la Bwana ulioimbwa na Hasheem Said.”
MSAGA SUMU
“Siku hiyo Msagasumu atakuwa moto wa kuotea mbali jukwaani ambapo ataimba na mashabiki pamoja ngoma zake zote kali kama vile Kijoti Joti huku mashabiki wa Simba na Yanga wakipata ladha ya kipekee kwa wimbo unaotikisa kila shoo za vigodoro wa Naipenda Simba na nyingine nyingi.”
MASAI WARRIORS
“Mapema kuanzia asubuhi kutakuwa na kundi zima la Masai Warriors ambapo litatoa burudani kwa watoto wote kama vile kucheza sarakasi, mashindano ya kuimba, kuvuta kamba, kucheza kwenye gunia na mingine mingi.
“Burudani pia itapatikana kwa watoto wote kama vile kubembea, kuteleza, kuogelea na watoto watakaopendeza wataondoka na zawadi kemkem.”