KWAKO mkali wa Bongo Fleva, Khaleed Mohamed ‘TID’ mambo vipi mzee? Kitambo kidogo sijakutia machoni. Mara nyingi nakuona kupitia vyombo vya habari. Naamini u-mzima wa afya.Ukitaka kujua hali yangu, mimi pia sijambo naendelea na mishemishe za mjini si unajua mjini mipango, tupo kama kawa.Mazungumzo baada ya salamu hizo, nataka nikupe dhumuni la barua hii. Nimekuandika barua hii nikiwa na mambo mawili ya msingi.La kwanza kabisa ni kukumbusha juu ya umuhimu wako katika jamii kama msanii maana wewe ni binadamu, yawezekana umepitiwa kidogo, kukumbushana muhimu.
TID wewe ni chachu ya mafanikio ya muziki wa Bongo Fleva. Wewe ni miongoni mwa wasanii ambao pia walileta mapinduzi katika suala zima la uigizaji.Kupitia sinema ya Girlfriend, ambayo ni miongoni mwa sinema za kwanzakwanza Bongo, ulionesha uwezo mkubwa sana katika kuigiza.
Ulichangia mapinduzi ya muziki na hata filamu. Heshima yako ni kubwa hivyo Watanzania wengi wapo nyuma yako. Wapo wenye ndoto za kuwa kama wewe hivyo endapo ukionesha matendo yasiyofaa, hauwezi tena kuwa mtu wa kuigwa na hao walio nyuma yako.
Hapo ndipo linapokuja suala zima la kujitambua. Niliposikia umetajwa katika tukio la kumshambulia mtu mwishoni mwa wiki iliyopita, nilishtuka sana. Nilishtuka kwa sababu akili yangu ilirudi nyuma katika tukio lako la kumpiga mtu lililokuweka katika wakati mgumu.
Nilikumbuka kwamba tukio hilo lilikufanya utupwe jela baada ya kupandishwa kizimbani na kupatikana na hatia hadi pale ulipokuja kuachiwa kwa msahama wa rais. Nilipopata taarifa hizo, nikajiuliza vipi tena TID yuleyule atende kosa linalofanana na lile ambalo lilisababisha afungwe? Kuna tatizo gani linalokusumbua katika masuala ya ugomvi?
Maswali hayakuishia hapo, nikajiuliza kweli unashindwa kujizuia hasira kiasi cha kunyanyua mikono yako na kuanza kumtwanga mwenzako makonde? Kila mmoja ana hasira tunapaswa kuwa wastaarabu. Mara zote jitahidi kadiri uwezavyo ili kuepusha dhahama yoyote mbele yako.
Unapokuwa mtu mwenye ‘taito’ kwenye jamii ndivyo unavyotakiwa kuongeza busara mara mbili zaidi za yule mtu wa kawaida. Watu wanaamini wewe ni kioo cha jamii sasa unapohusishwa na makosa ya kuvunja amani, raia wa kawaida unadhani watajifunza nini kutoka kwako?
Mbaya zaidi umri sasa unakwenda, yale mambo ya kuamini bado wewe ni kijana yanapitwa na wakati. Hiki kipindi si kile cha kuvaa ‘kata K’ na kuweka kitambaa kikubwa kikining’inia mfuko wa nyuma. Ni wakati wa wewe kuwaonesha watu kwamba ni mkongwe.
Wasanii wachanga waone mafaniko yako. Jitahidi sana kukaa mbali na matukio ya ajabu, yanakuvunjia heshima wakati wewe unaheshimika.
Boresha nyendo zako ili watu wasizitilie shaka. Onesha umekua, fanya mambo makubwa zaidi na watu wawe na hamu ya kukufikia.Bila shaka utakuwa umenisoma na nina imani utabadilika. Kwa leo naishia hapo, nitakuandikia tena barua pale itakapobidi.