Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete
ALMASI JUMA, MWANZA
Napenda kukupongeza Mh. Rais Kikwete kwa kazi nzuri uliyoifanya katika kipindi chote tangu ulipochaguliwa kwa kuwa kazi ya kuongoza nchi siyo jambo dogo. Ukitazama kipindi ulipoingia madarakani mpaka sasa ni mambo mengi mazuri umeyafanya kwenye uongozi wako likiwemo suala la kuongeza ajira kwa vijana. Hongera sana.
HALIMA PRIVER, ZANZIBAR
Sioni haja ya kuwaunga mkono wale wanaokubeza kwa kuwa umejitahidi kadiri ya uwezo wako kuboresha mambo mbalimbali katika nchi hii, hata huku kwetu upande wa visiwani tuna mengi ya kujivunia likiwemo suala zima la uboreshaji wa kivuko na kumaliza matabaka yaliyokuwa yameanza kujitokeza lakini kubwa zaidi ni kudumisha muungano. Hongera rais wangu.
SALUM SAID, DAR
Mheshimiwa Rais JK napenda kukupongeza kutokana na sapoti yako kubwa unayoionesha kwa wasanii. Mimi binafsi navutiwa sana na kazi za wasanii wetu wa hapa nyumbani na kwa kipindi chote katika uongozi wako umekuwa bega kwa bega kuwaunga mkono wasanii wetu waweze kusonga mbele na kujulikana kimataifa, mfano mzuri ni msanii Diamond. Bila msaada wako asingefika hapa alipo, nakusifu kwa hilo.
EMMANUEL KESSY, MOSHI
Kweli Rais JK yapo mambo ambayo umejitahidi sana kuyatekeleza ingawa yapo pia mapungufu katika utawala wako. Kwa mfano baraza lako la mawaziri asilimia kubwa halikuwa na sifa zinazostahili ndiyo maana ilikulazimu kulibadili mara kwa mara chanzo kikubwa kikiwa ni ufisadi uliokithiri wa hawa mawaziri wako.

Kwa hali kama hii ni dhahiri kwamba chama chako tayari kimeishiwa viongozi wenye sifa stahiki na hata serikali ijayo mkibahatika tena kuichukua hii nchi, mawaziri wabadilishwe kwani hawa uliowachagua wewe ndiyo waliosababisha chama chenu kionekane hakifai.
ZUWENA MANASE, DAR
Uongozi ni kitu kikubwa sana, wengi wanachukulia kitu chepesi kukaa ikulu, mazito yaliyomo huko wewe ndiyo unayajua. Nakupongeza kwa kusimamia ujenzi wa barabara za mwendo kasi japo mpaka sasa tunaona azma yako ya kumaliza madaraka ukiwa umezikamilisha na kuanza kutumika haitatimia kwa wakati. Binafsi nakupongeza.
DONALD MASAWE, MOSHI
Mpaka sasa bado najiuliza ni kiongozi gani mwenye busara na hekima kama zako anayeweza kuongoza nchi hii baada ya wewe kuondoka madarakani? Naweza kukufananisha na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kwa kuwa muda mwingi umeonekana ni mtu mwenye kutabasamu. Naamini hiyo ni moja ya sababu ya Mungu kutuletea mabadiliko kwenye nchi yetu kutokana na amani ya moyo uliyonayo.
HALIMA KUSAGA, TANGA
Ni mengi ambayo ulituahidi kipindi unaingia madarakani, siwezi kukupa sifa za moja kwa moja kwa kuwa kuna machache umeyatendea haki na mengine bado yamebaki kuwa kero likiwemo suala zima la maji huku vijijini bado ni tatizo.
MOHAMED JUMANNE, DAR
Pole sana Rais JK kwa kazi kubwa unayoifanya pamoja na misimamo yako uliyonayo. Mfano mzuri katika lile sakata la Escrow, uliweza kuwawajibisha wote waliohusika kwa kutumia busara za hali ya juu. Nimekuwa nikifarijika sana na hotuba zako ambazo huwa zinatutia nguvu wanyonge na kutufanya tusimame imara. Mimi nakuunga mkono kwa kuutendea haki uongozi wako kwa kuwa tulipotoka na tulipo sasa tumepiga hatua kubwa mno.
RASHIDI SALUM, KONDOA
Kuna mengi mazuri uliyoifanyia nchi hii, siwezi kuwaunga mkono wachache wanaokukwamisha kwenye mipango yako ya kujenga taifa, wewe ni kiongozi imara unayejiamini na ndiyo maana ukaweza kujenga ukaribu na viongozi wa nchi mbalimbali na kilichonivutia zaidi ni kitendo cha kumleta Rais wa Marekani, Barack Obama kutembelea nchi yetu.