Waziri wa Mambo ya  Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,  Bernard Membe akitoa tamko.
…Akisisitiza jambo.
Sehemu ya wanahabari na wageni wengine waliofika kwenye hafla hiyo.
WAZIRI wa  Mambo ya  Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amesema kuwa hakuna  Watanzania waliouawa nchini Afrika Kusini kutokana na machafuko yanayoendelea nchini humo.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Membe amesema kuwa serikali itawarudisha watu 21 tu ambao wamepata matatizo ya kuvamiwa  na ambao wako Ubalozi wa Tanzania wakiwa wamehifadhiwa.


Alisema kuwa serikali kamwe haitamrejesha Mtanzania yeyote  ambaye atatumia machafuko hayo yanayoendelea nchini humo kama njia ya kurudi Tanzania, kwani wapo Watanzania wengi wako huko na hawana vibali vya kuishi nchini humo.
Vilevile, alisema kuwa jambo ambalo serikali inasubiri kwa sasa ni kupata ruhusa kutoka ubalozi huo ili kuwarejesha Watanzania hao  waliokubali kurudi nyumbani.
Membe amekanusha  taarifa zilizokuwa zikiripotiwa kwenye mitandao ya kijamii  na baadhi ya vyombo vya habari  vikidai kuwa Watanzania watatu wamefariki kutokana na machafuko hayo.  Alisema Watanzania hao watatu wamefariki kutokana na magonjwa na si kwa sababu ya machafuko hayo
 
Amewataja watu hao kuwa ni Athumani China ambaye amekufa kutokana na kupigwa na wananchi wenye hasira baada ya kumpora mzawa wa huko.  Mwingine ni Ally Mohamed aliyefariki kutokana na kifua kikuu, na mwingine aliyefia gerezani.
Waziri huyo amewataka Watanzania waishio nje ya nchi kupendana na  kuwa pamoja ili matatizo kama hayo yanapotokea iwe rahisi kwa serikali kutoa msaada.