Mwenyekiti wa Chama cha TLP, Augustine Mrema (aliyebeba bendera) akiongoza maamdamano ya wafuasi wa chama hicho kuelekea katika Ukumbi wa King Palace uliopo Sinza, Dar es Salaam ulipofanyika mkutano mkuu wa chama hicho, jana. Picha naSaid Khamis
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema amedai kuwa serikali iliyopo madarakani imeshindwa kazi kutokana na mawaziri na watendaji wengine kumwachia majukumu yote Rais Jakaya Kikwete.
Akizungumza wakati wa mkutano mkuu wa uchaguzi wa chama hicho uliofanyika Dar es Salaam jana, Mrema alisema kuna mambo mengi ya ajabu yanayojitokeza katika ofisi za Serikali yanayokatisha tamaa wananchi.
Mrema alisema karibu kila sekta ikiwamo ya ulinzi na usalama, zinayumba na mbaya zaidi wasaidizi wa Rais bado hawajaweza kufanya kitu chochote kuikabili hali hiyo.
“Nchi inaelekea kubaya, kuna matatizo mengi ya kiusalama ambayo hayana majibu, kuna masuala ya ugaidi, udini, mauaji ya albino, uvamizi, uporaji wa silaha na mauaji katika vituo vya polisi,” alisema.
Mrema aliyataja matukio mengine kuwa ni migomo ya madereva na wafanyabiashara na alisema yote hayo yanatokea, hakuna kiongozi hata mmoja ambaye amejitokeza kuyashughulikia kikamilifu, kila mmoja anasubiri Rais Kikwete aseme neno au achukue hatua.
“Serikali imeshindwa kazi, hakuna mtu wa kumsaidia Rais,” alisema Mrema na kuongeza kuwa wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Naibu Waziri Mkuu, Waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) walikuwa wanachinjana, makanisa yanachomwa lakini alijitolea kupambana na mgogoro huo na alifanikiwa kuumaliza.
Mkutano huo ulihudhuriwa na wajumbe 86 kutoka mikoa 17 nchini, kiwango ambacho Makamu Katibu Mkuu wa Chama hicho, Nancy Mlekeria alisema inakidhi akidi na hivyo kuufanya kuwa halali.
Ofisa Sheria wa Msajili wa Vyama vya Siasa, Monica Mwailolo alisema umefuata taratibu zote kulingana na Katiba ya TLP na utachagua mwenyekiti, makamu wa Bara na Zanzibar na pia utamtangaza mgombea Urais katika Uchaguzi Mkuu ujao kupitia TLP.
|
0 Comments