Askari wakiondoa vizuizi barabarani vilivyowekwa na wananchi waliojichukulia sheria mkononi eneo la Stendi Kuu ya ipogolo baada ya ajali. Picha na Saidi Ngamilo 
Dar/Iringa/Dodoma. 
Watu watano wamefariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa katika mikoa ya Dodoma na Iringa ikiwa ni muda usiozidi saa 24, baada ya kumalizika mgomo wa madereva wa mabasi na malori.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, jana alithibitisha kutokea kwa ajili hiyo ya Dodoma, saa 3:45 usiku, katika eneo la Nzuguni nje kidogo ya mji wa Dodoma.
Alisema basi hilo lilikuwa likitokea Mwanza kwenda Morogoro liligongana na gari ndogo aina ya Toyota Mark II iliyokuwa likiingia barabara kuu kutokea Nzuguni.
“Chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa gari dogo kuingia barabarani bila kuwa makini na kusababusha kushindwa kumpa kipaumbele aliyekuwa barabara kuu kupita kwanza.
“Lakini pamoja na makosa ya gari ndogo, suala la mwendo kasi wa dereva wa basi umesababisha madhara kuwa makubwa,” alisema.
Aliwataja waliopoteza maisha ambao wote ni waliokuwa katika gari ndogo kuwa ni Askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), Monduli mkoani Arusha, Jackson Lazaro aliyekuwa dereva wa gari dogo.
Wengine waliofariki katika ajali hiyo ni  Mkazi wa Makole, Helena Chiuyo (36), Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya City ya mjini hapa, Fatuma Mtauga (17) na Mkazi wa Kisasa Stella Giseon (36).
“Dereva wa gari dogo alikuwa akitokea kijiji Nzuguni kuingia barabara kuu ya Dodoma kuelekea Morogoro kugongana basi ambalo lilipoteza mwelekeo na kuingia porini umbali usiopungua mita 300 na kugonga mti na kisha kusimama,”alisema Kamanda Misime.
Alisema dereva wa basi ambaye ni Mkazi wa Kirumba Mwanza, Leonard Magesa (51) anashikiliwa na polisi kwa mahojiano.
Naye Ofisa Muuguzi wa zamu katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma, Cecilia Sanya,  alisema alipokea majeruhi huyo saa 6.20 Fatuma Patrick kutoka eneo la ajali akiwa majeraha sehemu mbalimbali za mwili ikiwemo kichwani .
“Waliongoza na wauguzi wa zamu kwenda katika eneo la tukio wakiwa na gari la wagonjwa, walivyofika pale walikuta watu hao wamefariki dunia,” alisema Cecilia.
Naye mmoja wa mashuhuda,  Christian Kihonda, alisema dereva wa basi alikuwa katika mwendo kasi baada ya mgomo kumalizika juzi mchana.Ajali ya Iringa
Polisi mkoan Iringa ililazimika kuwatawanya kwa mabomu ya machozi wakazi wa eneo la Ipogolo na wengine kupigwa vibaya na kufikishwa katika Kituo cha Polisi baada mwanafunzi wa shule ya Sekondari Isimila aliyefahamika kwa jina la Hamfrey Ng’amilo kugongwa na gari na kufariki dunia papo hapo.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi mkoa wa Iringa,  Ramadhani Mungi alisema ajali hiyo ilitokea jana saa nane mchana ambapo gari gari aina ya Toyota Coaster mali ya Mwandago Investment iliyokuwa ikiendeshwa na Ismail Burhan ilimgonga mwanafunzi huyo na kupoteza uhai wake.
Mungi alisema kuwa dereva wa gari hiyo alikuwa ni fundi magari na alikuwa anaifanyia majaribio gari hilo baada ya kumaliza kutengeneza.
 “Coaster hiyo inafanya safari zake kati ya Iringa na Arusha hivyo ilikuwa mbovu na ilikuwa gereji kwa ajili matengenezo na wakati akilijaribu, alipofika maeneo ya Ipogolo Stendi ndipo alimgonga mwanafunzi huyo,” alisema Mungi.
Kwa upande wake ndugu wa marehemu Said Ng’amilo ambaye ni mpiga picha wa gazeti la Mwananchi alisema kuwa alipatwa na mshtuko baada ya kufika katika eneo hilo kwa ajili ya kupiga picha na kukuta aliyegongwa katika ajali hiyo ni mdogo wake.
“Kiukweli huyu marehemu ametokea katika kijiji jirani cha Ikuvilo ambako ndiyo nyumbani alikuja kunyoa nywele kwa ajili ya maadalizi ya kurudi shule na sikuwa na taarifa kuwa yupo mjini nimethibitisha baada ya kupiga simu kijijini na kuambiwa alikuwa likizo ya Pasaka na amekuja mjini kunyoa nywele na kesho alitaraji kurudi shule,” alisema Ng’amilo
 Mmoja wa wakazi hao aliyefahamika kwa jina la Fatuma Ally alisema kuwa waliamua kufunga barabara na kuchoma matairi baada ya mwili wake kukaa barabarani kwa mda mrefu bila kuchukuliwa licha polisi kupewa taarifa ya tukio.
Mnadhimu wa Polisi alonga
Mnadhimu Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Johanes Kahatano amesema wanasubiri kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani kuhusu kubatilishwa kwa kanuni mpya za usalama wa barabarani.
Juzi Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka alitoa kauli ya kutengua matumizi ya kanuni mpya, zilizokuwa zinawataka madereva kwenda Chuo cha Usafirishaji (NIT) kwa mafunzo ya muda mfupi baada ya miaka mitatu ya leseni na ndiyo njia ya kupata leseni nyingine.
Hata hivyo, akizungumzia uamuzi huo jana, Kamishna Kahatano alimwambia mwandishi wa gazeti hili kwamba:“Aliyetoa kauli ile siyo waziri husika licha ya kumwakilisha Waziri wa Mambo ya Ndani, kwa sasa tunasubiria kauli kutoka kwa waziri husika ambaye ndiyo mwenye mamlaka ya kuhuisha sheria,” alisema Kamishna Kahatano.
Alipoulizwa juu ya agizo la kuzuia matumizi ya tochi, Kamishna Kahatano alisema bado ni sehemu ya juhudi ambazo zimekuwa zikisaidia kupunguza ajali za barabarani.
 “Lakini kuhusu ajali zilizotokea leo sina hakika kama kuna uhusiano na tukio la mgomo wa jana,” alifafanua Kahatano juu ya ajali mbili zilizotokea jana Iringa na Dodoma baada ya kutokea mgomo huo.
Kwa upande wake, Msemaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), David Mziray alisema kauli ya Waziri Kabaka haikutolewa kisiasa bali ilikuwa inalenga kutafuta ufumbuzi wa dharura ili kunusuru changamoto iliyokuwa imejitokeza kwa taifa.
Hata hivyo, Mziray alisisitiza umuhimu wa kanuni hizo akisema ni miongoni mwa hatua zinazoendelea kuchukuliwa ili kupunguza ajali za barabarani.
Alisema Sumatra imekuwa ikitoa miongozo na kufanya tathmini huku ikipokea tafiti mbalimbali zinazoonyesha vyanzo vya ajali nyingi kuhusishwa na makosa ya kibinadamu.
“Kwa hivyo hatuwezi kuepuka kanuni hizo labda zifanyiwe maboresho tu kwa kiwango fulani kama suala la kupunguza ada za malipo na vitu vingine, siyo biblia hiyo lakini siyo kufutwa,”alisema Mziray.
*Imeandikwa na Sharon Sauwa, Berdina Majinge na Kelvin Matandiko.