Na Elvan Stambuli
MWENDO  wa Kiongozi Mkuu wa Alliance for Change and Transparency (ACT) Wazalendo, Zitto Zuberi Kabwe (pichani) umetafsiriwa kuwa ni wa spidi 160 kutokana na kujawa wasikilizaji katika mikutano yake anayofanya kwenye  mikoa mbalimbali nchini.

Kiongozi Mkuu wa Alliance for Change and Transparency (ACT) Wazalendo, Zitto Zuberi Kabwe.
Zitto ameshafanya mikutano katika Mikoa ya Ruvuma, Njombe, Morogoro, Shinyanga na Mwanza na mikutano yake imekuwa ikihudhuriwa na wananchi wengi, hivyo kutumia mwanya huo kugawa kadi za chama chake.
Alipohojiwa na gazeti hili kuhusu hali hiyo ya kujaza watu, Zitto alisema mwendo wa chama chake ni kama moto wa pumba ambao ukiwa unauangalia kwa juu, utadhani umezimika lakini ukiingiza mguu, unaungua.
“Sisi tunafanya kazi usiku na mchana ili kupata wanachama ili uchaguzi mkuu ukifika tupate wabunge wa kutosha,” alisema Zitto aliyewataka wananchi kujiandikisha muda ukifika pale Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) itakapowafikia kuwaandikisha.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa alipoulizwa kama spidi 160 anayokwenda nayo Zitto haiwezi kuwa tishio kwa chama chake, alisema Chama cha ACT Wazalendo hakiwezi kukitisha chama chake hata kidogo.
 Dk. Slaa aliongeza: “Chadema tumeijenga kuanzia ngazi za chini kwa miaka mingi, hatumuogopi yeyote. Dk. Slaa, Mbowe na timu nzima tumezunguka Tanzania nzima kijiji kwa kijiji, hivyo hakuna mtu yeyote atakayekuwa tishio kwetu.” 
Akizungumzia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), alisema  imekuwa ikilalamikiwa kuhusiana na kuchelewa kuletwa kwa mashine za mfumo wa Biometric Voters Registration ( BVR), lakini dosari ya msingi katika suala la BVR ni serikali kushindwa kutoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa hivyo.
Dk. Slaa alisema Agosti 30 na Septemba 8, mwaka jana, viongozi wa vyama vya siasa nchini walikutana na Rais Jakaya Kikwete na wakajadiliana masuala kadhaa likiwamo la uandikishaji wa Daftari la Wapiga kura kwa kutumia mfumo mpya wa BVR  na kukubaliana kuwa mambo ambayo siyo ya kikatiba na yasiyo ya lazima yasifanyike kwanza katika kipindi hiki ili kupunguza gharama.
Dk. Slaa ambaye amerejea hivi karibuni kutoka Marekani, alisema miongoni mwa mambo waliyoyaomba yasifanyike kwanza ni kura ya maoni kwa ajili ya Katiba Inayopendekezwa kwa kuwa siyo jambo la kikatiba, lakini katika hali ya kushangaza serikali ikatangaza tarehe ya kufanyika kura ya maoni licha ya kuwapo makubaliano hayo.
 “Rais Kikwete alikubali na kupendekeza kuahirishwa kura ya maoni hadi baada ya uchaguzi mkuu ili kuokoa fedha ili zitumike kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu, lakini hilo halikuzingatiwa,” alisema.
 Aliongeza kuwa hadi sasa serikali imetumia fedha nyingi sana kufanya kampeni kwa ajili ya kura ya maoni na cha kushangaza ni kuwa serikali ndiyo inayofanya kampeni badala ya wananchi .
Dk. Slaa alisema wamebaini kuwa kuandikisha wapiga kura kwa kutumia  BVR ni mbinu inayofanywa na serikali kwa sababu kuna maeneo ambayo wananchi hawataandikishwa na ndiyo maana wameanza maeneo ambayo ni ngome za Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Tunataka kuwaambia kuwa tumeshtukia na tunatoa rai kwa Rais Kikwete, nchi hii ni muhimu kuliko yeye, nchi ni muhimu kuliko CCM na kuliko Chadema, hata siku moja upinzani hauwezi kuleta vurugu, vurugu zitaletwa na serikali yenyewe inayotaka kulazimisha mambo yake,” alisema.