Staa wa muziki wa Pop duniani, Shaffer Chimere Smith ‘Ne-Yo’ akiwa na Ally Kiba.
UNAANDIKA lakini? Ni moja ya misemo iliyozagaa sana mtaani kwa sasa, msemo huu hupendelewa kutumiwa zaidi pale mtu anapoongea sana au anapokuwa bize kukwambia jambo fulani kwa msisitizo.
Julai 18, mwaka huu staa wa muziki wa Pop duniani, Shaffer Chimere Smith ‘Ne-Yo’ alitua katika ardhi ya Afrika na moja kwa moja alipata bahati ya kuhudhuria sherehe za utoaji Tuzo za MTV Africa (Mama) zilizofanyika jijini Durban, Afrika Kusini.
Ne-Yo akiwa na Nasibu Abdul ‘Diamond’.
Diamond
Ujio wa Ne-Yo Afrika ulikuwa bahati sana kwa staa wa Afro Pop, Nasibu Abdul ‘Diamond’ kwani licha ya kukutana naye hapo awali nchini Marekani kwenye sherehe za utoaji Tuzo za BET safari hii aliweka dhamira ya kufanya naye kolabo.

Hivi karibuni, Diamond alikwea pipa hadi nchini Kenya kufanya kolabo hilo akiwa na meneja wake, Salam pamoja na Prodyuza Sheddy Clever na tayari kila kitu kimekwenda sawa bado kutoka kwa wimbo tu.
Ali Kiba
Kama ilivyo kwa Diamond, hivi karibuni staa mwingine wa Afro Pop, Ally Saleh ‘Ali Kiba’ alikuwa mmoja kati ya wasanii wa Afrika Mashariki watakaofanikisha msimu mwingine wa Coke Studio akiwa sambamba na Benard Paul ‘Ben Pol’.
Kupitia fursa hiyo iliyojitokeza nchini Kenya, Ali Kiba kama ilivyokuwa kwa Diamond amefanikisha kuingia studio na kutengeneza kolabo la nguvu na Ne-Yo na kwa sasa kinachosubiriwa kutoka kwa wimbo tu.
Mnaandika lakini?
Macho na masikio ya mashabiki wengi wa muziki huu yameelekezwa kwa mastaa hawa. Wengi wanajiuliza kolabo ipi itakuwa bomba na wengine wamefika mbali zaidi kufikia video ipi itakuwa bomba.
Diamond na Ali Kiba, kwa muda mrefu mmeonekana kukomaa katika muziki huu wa Afro Pop kwa kufanya kazi nzuri zinazotambulika kimataifa ikiwa ni pamoja na kupiga kolabo na wasanii nyota wanaotambulika Afrika na nchi za ulaya kama vile, KCEE, R.Kelly, Bracket, Mr. Flavour, Iyanya, Donald na wengine kibao.
Tambueni kuwa Ne-Yo ni mmoja wa mastaa wanaokubalika duniani kwa kuwa na sauti ya kipekee. Moja ya sifa alizonazo ni kufanya muziki wa Euro Pop unaofanywa nchini Ujerumani, Italia, Ufaransa na kwingineko.
Sifa ya kipekee aliyokuwa nayo jamaa huyu, licha ya kuimba pia ni mwandishi mzuri wa mashairi kwani alishawang’arisha mastaa kibao kama vile Beyonce kupitia Wimbo wa Irreplaceable, Rihanna Wimbo wa Take a Bow, Let Me Love You wa Mario na wengine kibao kama Marry J. Blige, B2K na Faith Evans.
Huu ni wakati wa Diamond na Ali Kiba kutumia fursa hii ya kung’arishwa kwa kufanya kila liwezekanalo ili tu kolabo mlizofanya naye kufika mbali zaidi ikiwezekana kujua njia ya kufanya muziki wetu usikike na kukubalika nje ya Afrika.
Pia kupitia Ne-Yo inawezekana kabisa kupata fursa ya kuweka ukaribu na mastaa wa kiwango cha kimataifa kama vile Beyonce, Chris Brown, Lil Wayne, Rihanna, Drake na wengine kibao wakakubali kazi zenu.
Kolabo lenu na Ne-Yo liwe njia ya kutoboa zaidi na siyo kuishia Afrika pekee. Najua kama mtazingatia yote haya, sote pamoja tunaweza kujitengenezea mazingira mazuri Ulaya kuliko hata nchi za Nigeria, Ghana na Afrika Kusini zinazoonekana muziki wao kukua.
Nimeongea sana bila kuwauliza, Diamond na Ali Kiba mnaandika lakini?