WANANCHI wametakiwa siku ya kupiga kura kuwa macho na watu wanaoweza kwenda kuwanunua kwa kuwagawia fedha wabadilishe msimamo wao. Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli, alitoa hadhari hiyo jana mjini hapa kwenye mkutano wa kampeni uliohudhuriwa na maelfu ya watu.
Magufuli ambaye aliendelea kusisitiza kuwa mtu anayenunua watu hawezi kuona aibu kuuza haki zao, alisema zipo taarifa za wengine wanaonunua shahada ambao wananchi wanapaswa kuwa macho nao.

“Siku ya kupiga kura, kuna watu wanaweza kupita na kutoa fedha… ukiona mtu ananunua shahada, anatumia fedha kukununua, hataona aibu kukuuza, kwa maana ya kuuza haki yako ya maendeleo,” alisema.
Pia katika mkutano wa kampeni aliofanya mjini Kiomboi, Magufuli alisema, “nimesikia tayari kuna watu wanaanza kupita na kununua shahada na wengine wanapita wanatoa hela. Hela kuleni lakini kura pigeni kwa CCM.”
Akiahidi kusimama imara na kulinda maslahi ya Watanzania, alisisitiza namna ambavyo kwenye mchakato wa kampeni kwenye kura za maoni, hakuna aliyekula fedha yake. Katika hatua nyingine, Mkoa wa Singida umeahidiwa neema ya kujengewa hospitali itakayohudumia mikoa ya Kanda ya Kati na mingine iliyo jirani ambayo itakuwa kubwa kama ilivyo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Aidha Dk Magufuli, ameahidi mkoa huo utapata uwanja mkubwa wa ndege utakaopanua wigo wa usafiri kwenda mkoani humo. “Nataka hospitali ya Kanda itakayojengwa Singida iwe kubwa kama Muhimbili.
Mikoa yote ya jirani wafike kutibiwa hapo.” Alimpongeza Mkuu wa Mkoa Singida, Dk Parseko Kone kwa kusimamia mchakato huo kuhakikisha hospitali hiyo inajengwa. Wakati huo huo Magufuli alimpongeza aliyekuwa Mbunge wa Singida Mjini, Mohamed Dewji na akisema anapenda wawekezaji wazalendo wanaoipenda Tanzania.
Alimuahidi kumpa ushirikiano atakapohitaji kuwekeza. “Na wewe kama unapenda kujenga kiwanda chochote nitakuunga mkono…,” alisema Magufuli. Alimuomba atengeneze hata viwanda vitatu awezeshe wananchi wa Singida wapate ajira.
Nitakuunga mkono kwa asilimia 100 kama ni kibali unataka, nitakupa leo hii hii kwa kuwa mmenihakikishia nitakuwa rais,” alisema. Alisema mji wa Singida ni wa kibiashara hivyo atahakikisha unakuwa na lami kwenye barabara za ndani.
Kuhusu uwanja wa ndege, alisema utawezesha wawekezaji wanaotaka kuja kwa ajili ya biashara, wapate fursa ya kutumia usafiri wa anga.