JUKWAA la Katiba Tanzania (JUKATA) limepongeza uteuzi wa Waziri Mkuu uliofanywa na Rais John Magufuli kwa kumteua Mbunge wa Ruangwa, Kassim Majaliwa.
Mwenyekiti wa jukwaa hilo, Deus Kibamba alisema Rais amefanya uteuzi sahihi kwani waziri huyo ni miongoni mwa watu wasiokuwa na makandokando ya ufisadi na wala rushwa. Kibamba alisema wanaamini kuwa Majaliwa atasaidia katika kutatua kero za wafanyakazi kwa kuwa aliwahi kuwa mwalimu na kwamba anajua matatizo yanayowakabili wananchi.
‘’Haya ni mageuzi makubwa aliyoyaahidi kwa kuanza na kuunda kikosi cha miavuli kwa kuanzia na Waziri Mkuu makini na mchapakazi,’’ alisema Kibamba akimzungumzia Majaliwa ambaye katika Serikali ya Awamu ya Nne, alikuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa akishughulikia Elimu.
Aidha, Kibamba alisema suala la Rais kuhutubia Bunge pasipo kuwepo kwa wawakilishi kutoka Zanzibar, haliwezi kuwa kikwazo kwani Katiba ya mwaka 1977 inaweka wazi kwamba Rais anaweza kuhutubia Bunge hilo pasipo wabunge na wawakilishi wengine kuwepo.
Alisema Rais hawezi kuahirisha kuhutubia Bunge kutokana na majimbo machache kutofanya uchaguzi au wawakilishi kutokuwepo. Aidha, Jukata ilimuomba Rais Magufuli kumteua aliyekuwa mgombea urais kupitia chama cha ACT-Wazalendo, Anna Mghwira kuwakilisha wananchi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Kwanza tunampongeza Mghwira kuwa ni mwanamke pekee ambaye aliendesha kampeni zake kwa hoja na sera bila ya kutumia lugha ya uchochezi, hivyo tunamuomba Rais amchague (kupitia nafasi zake 10) ili akawakilishe wananchi,’’ alisema Kibamba.
Kuhusu mchakato wa Katiba mpya, Jukwaa limemwomba Dk Magufuli kutangaza rasmi namna ya kurejea kwenye mchakato huo na kwamba atumie mamlaka yake kuonesha jinsi ya kutoka kwenye mkwamo huo.
Jukwaa hilo pia limemuomba Rais kuongoza jitihada za kuinusuru Zanzibar kwa kutambua kuwa hatua ya Umoja wa Serikali ya Kitaifa iliyokuwa imefikiwa na Wazanzibari inapaswa kulindwa na kuheshimiwa.
|
0 Comments