RAIS wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli amefungua Bunge la 11 na kuwataka watendaji kote nchini kuhakikisha wanashiriki katika vita ya kuondoa umasikini, ili ukuaji wa uchumi wa nchi uendane na ukuaji wa uchumi wa watu na kusisitiza kuongeza ajira kupitia viwanda.
Akihutubia bungeni jana mjini hapa, Dk Magufuli alisema kwa kuwa hakuna viwanda vingi vinavyotoa ajira, kwa kuanzia watendaji wote wanatakiwa kuacha unyanyasaji kwa wafanyabiashara ndogo, wakiwemo mamalishe, machinga na bodaboda.
Akifafanua amesema biashara hizo ndogo, ndizo zinazosaidia vijana kuacha kujiingiza katika vikundi viovu na kujikita katika utafutaji wa kipato, huku akiongeza kuwa baadhi ya watendaji wakinyang’anya mama lishe chakula, wamekuwa wakivila.
“Tulifanye hili kwa kuondoa kodi na ushuru usiokuwa wa lazima kwa wafanyabiashara wadogo hawa. Unakuta mama ntilie ananyang’anywa vyakula vyake, halafu wanaovichukua wanakula wenyewe. Inakera kweli.
“Tuwatengee maeneo ya kufanya biashara, tupunguze kodi, badala ya kuwasumbua wakati wanajitafutia riziki,” alisema Dk Magufuli.
Mbali na agizo hilo la kutosumbua wafanyabiashara ndogo, Dk Magufuli aliahidi kusimamia sekta ya viwanda katika kilimo, mifugo na uvuvi, ili kuongeza thamani ya mazao na kipato cha wakulima, wavuvi na wafugaji na ajira na kwamba anataka hadi mwaka 2020, asilimia 40 ya ajira itokane na viwanda vinavyohusika na kilimo, uvuvi na mifugo.
“Hili ni eneo ambalo katika kampeni zangu nilitumia muda mwingi kulielezea sana, nataka kuhakikisha tunaondoa umasikini na kuongeza ajira,” alisema Dk Magufuli.
Alisema eneo hilo la viwanda atalisimamia kwa kuhakikisha viwanda vilivyobinafsishwa lazima viendelezwe na kama wahusika wakishindwa wajiandae kuvirudisha serikalini, lakini pia serikali ikifanya mpango wa kuanzisha viwanda vipya vinavyotokana na mifugo, kilimo na uvuvi.
Katika viwanda vipya, Dk Magufuli alisema Serikali yake itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na kupunguza urasimu serikalini huku akionya watendaji ambao wamekuwa wakizungusha wawekezaji, mpaka wanaamua kwenda kuwekeza katika nchi jirani, kwamba atawatimua mara moja.
Dk Magufuli alisema pia atahakikisha umeme unakuwa wa kutosha na wa uhakika, kwa kuwa hawezi kuzungumzia viwanda wakati hakuna umeme wa kutosha, huku akionya watendaji wa Shirika la Umeme (TANESCO), ambao wamekuwa wakihujumu miundombinu ya umeme, baada ya kuhongwa na wafanyabiashara wa majenereta na wanaouza mafuta.