RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema ushindi wa tuzo ya dhahabu iliyopewa Sheria ya Watoto ya Zanzibar ni kielelezo cha matokeo ya kazi nzuri iliyofanywa na wengi kwa maslahi mapana ya watu wa Zanzibar.
“Ni umoja na mshikamano wetu uliotuwezesha kushirikiana wakati wote wa kutayarisha sheria hii pamoja na mkakati wake wa utekelezaji ndio uliotupatia zawadi hii adhimu kwa nchi yetu,” alisema Dk Shein.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo na Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana na Watoto, Zainab Omar Mohamed ofisini kwake Ikulu jana, Dk Shein alisema tuzo hiyo ni fahari kubwa kwa wananchi wa Zanzibar na inadhihirisha azma ya serikali kuhakikisha ulinzi na ustawi wa watoto unakuwa wa kiwango cha kimataifa.

Zanzibar ilitunukiwa tuzo hiyo ya Gold Future Policy Award kwa mwaka 2015 na kukabidhiwa mjini Geneva, Uswisi, Oktoba 20, mwaka huu baada ya Sheria ya Watoto ya Mwaka 2011 kuzishinda sheria za nchi nyingine zaidi ya 20 kwa kukidhi vigezo vinavyoshindaniwa.
Alisema wapo wanaoiunga mkono sheria hiyo, lakini alitahadharisha pia kuwa wapo wanaoipinga kwa dhahiri na wengine kwa kujificha, lakini kitu muhimu ni kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano ili sheria hiyo itekelezwe na kufikia malengo ya kupitishwa kwake.
Alisema kutokana na sifa iliyopata sheria hiyo, mwezi ujao Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Philip Marmo atawasilisha mada kuhusu sheria hiyo katika kongamano litakalofanyika Hamburg, Ujerumani.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Asha Ali Abdallah alisema ilitolewa na Taasisi ya Kimataifa ya World Future Council inayoshughulikia kuhamasisha uandaaji na utekelezaji wa sera zinazolenga kuimarisha ustawi, haki na hali za maisha kwa vizazi vya sasa na vijavyo.