TAASISI ya masuala ya jamii ya Vodacom Foundation imetoa msaada wa vifaa vya elimu kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Chazinge A, Kisarawe mkoani Pwani. Vifaa hivyo ambavyo vimetolewa jana ni madaftari ya kuandikia na mikebe yenye vifaa vya kusomea somo la hisabati pamoja na kalamu.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada wa vifaa hivyo kwa wanafunzi jana, Kaimu Ofisa Mkuu wa Mawasiliano na Uhusiano wa Vodacom Tanzania, Rosalynn Mworia alisema elimu ni moja ya kipaumbele ambacho taasisi hiyo inatoa na vipaumbele vingine vikiwa ni kusaidia kuboresha sekta ya afya.
“Vodacom Foundation tunaelewa kuwa elimu ni ufunguo wa maisha na hakuna jamii ambayo inaweza kuendelea bila kutoa elimu kwa watu wake, ndio maana tumekuwa mstari wa mbele kuunga mkono jitihada za serikali za kuboresha sekta ya elimu nchini,” alisema Mworia.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake baada ya kupokea msaada huo, Aisha Salum anayesoma darasa la nne shuleni hapo alisema vifaa hivyo vitachangia kufanya vyema kwenye masomo yao.
|
0 Comments