KAMATI Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imemaliza kazi yake na sasa mgombea nafasi ya Spika kupitia chama hicho ni ama Job Ndugai, Abdullah Ali Mwinyi au Dk Tulia Ackson Mwansasu.
Pia Kamati Kuu imesema utaratibu iliotangaza awali wa namna ya kumpata Naibu Spika haukuzingatia Katiba na suala hilo linapaswa kushughulikiwa na Kamati ya Wabunge wa CCM, hivyo leo wataanza kutoa fomu kwa waombaji wa nafasi hiyo. Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati Kuu chini ya Mwenyekiti wa Taifa, Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Nape Nnauye alisema pia leo Kamati ya Wabunge wa CCM itapiga kura kuchagua jina moja kati ya hayo matatu yaliyoteuliwa jana.

Ndugai (55) ni Naibu Spika katika Bunge la 10 lililomaliza muda wake chini ya Spika Anne Makinda akishika nafasi hiyo tangu mwaka 2010. Amekuwa Mbunge wa Jimbo la Kongwa mkoani Dodoma tangu mwaka 2000 na alishinda tena katika uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka huu. Alitajwa kuwa mbunge mwenye mchango mkubwa katika Bunge la Tisa.
Dk Tulia aliyezaliwa Novemba 23, 1976 wilayani Tukuyu mkoani Mbeya, ni Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliyeteuliwa kushika wadhifa huo na Rais mstaafu Kikwete, Septemba 9, mwaka huu. Alikuwa Mjumbe wa Bunge la Katiba na ni mtaalamu katika sheria za hifadhi za jamii, kazi, uhifadhi wanyamapori, udhamini, sheria ya usimamizi wa mirathi, ufadhili miradi na madini.
Abdullah, ambaye ni mtoto wa Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi maarufu Mzee Ruksa, ni Mbunge wa Afrika Mashariki tangu mwaka 2007. Aliwania ubunge ndani ya CCM katika Jimbo la Kigamboni mwaka huu, lakini kura hazikutosha kumfanya apitishwe kupeperusha bendera.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuchukua fomu hizo wiki hii Dar es Salaam, Ndugai alisema ameamua kuwania nafasi hiyo kutokana na ukweli kuwa Bunge la 11 ni Bunge litakalokuwa na changamoto hivyo linahitaji Spika mwenye weledi, uvumilivu na uzoefu wa kutosha katika mambo ya kuongoza Bunge.
“Jina hilo moja litakalopitishwa, ndilo litakalopelekwa bungeni kwa ajili ya kupigiwa kura kuwania Uspika kwa tiketi ya CCM,” alisema Nape na kukataa kutaja vigezo walivyotumia kupata wateule watatu kati ya zaidi ya 20 walioomba nafasi hiyo zaidi ya kusisitiza wote ni wanachama wa CCM.
Wagombea wengine wa nafasi ya Spika ambao majina yao yameshindwa kupenya kwenye Kamati Kuu ni aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta, Mbunge wa zamani wa Mbulu ambaye amepata kuwa Waziri katika Awamu ya Kwanza ya Serikali ya Awamu ya Nne na pia aliyepata kuwa Balozi, Philip Marmo. Sitta alikuwa Spika wa Bunge la Tisa akijinasibu kuwa Spika wa Viwango na Kasi, lakini akakatwa mwaka 2010 alipojaribu kuwania tena kiti hicho.
Hii ni mara ya pili lake kutopitishwa kuwania kiti hicho, na mwaka huu hakuwania tena ubunge jimboni kwake Urambo Mashariki. Wengine waliokatwa ni Mbunge mteule wa Chato, Dk Medard Kalemani, Diwani wa Goba jijini Dar es Salaam, Mwakalika Watson, Julius Pawatila, Agnes Makune, aliyewahi kuwa Naibu Waziri, Ritha Mlaki na mhitimu wa chuo kikuu mwenye umri wa miaka 28, Veraikunda Urio na Meya wa zamani wa Dar es Salaam, Didas Masaburi.
Pia walikuwamo aliyekuwa Mbunge wa Karagwe, Gosbert Blandes na aliyekuwa mmoja wa wagombea takribani 42 waliojitokeza kuwania nafasi ya Urais ndani ya CCM, Dk Kalokola Muzzamil Mbunge wa zamani wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi; Balozi wa zamani wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu, Mbunge wa zamani wa Afrika Mashariki, George Nangale, Simon Rubugu, Banda Sonoko na Leonce Mulenda.
Akifafanua kuhusu Naibu Spika, Nape alisema ilifanyika makosa kusema nafasi hiyo itashughulikiwa na Kamati Kuu, badala yake kwa mujibu wa kanuni suala hilo linashughulikiwa na Kamati ya Wabunge wa CCM. “Kanuni za Kamati ya Wabunge wote wa Chama Cha Mapinduzi zimetungwa chini ya Ibara ya 104 (6) ya Katiba ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 1977, toleo la 2010, toleo la nne 2011.
“Ibara ya 57 inasema mwanachama wa CCM anayetaka kugombea nafasi ya Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, atajaza fomu maalum ya maombi na kuiwasilisha kwa Katibu wa Kamati ya Wabunge wote wa CCM katika muda uliowekwa.
Ada ya fomu hiyo itakuwa Sh 100,000 tu ambazo zitalipwa wakati mgombea anarudisha fomu kwa Katibu wa Kamati,” alisema Nnauye. Alieleza kutokana na hali hiyo wabunge wanaotaka kuwania nafasi hiyo watachukua fomu kuanzia leo kwa Katibu wa Kamati ya Wabunge wa CCM na mwisho wa kuirudisha ni kesho saa kumi alasiri, ambapo kutafanyika Uchaguzi wa Naibu Spika utakaofanywa na kamati ya wabunge wa CCM.
Kabla ya uamuzi huo wa Kamati Kuu, mgombea pekee aliyekuwa amejaza fomu kuwania nafasi hiyo alikuwa Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu. Akizungumzia vyama vingine kuhusu nafasi ya Spika, Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Ramadhani Kailima alisema majina ya watu 23 kutoka vyama sita vya siasa nchini yalipelekwa kwao yakiwemo kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa wale wasio wabunge.
“Kwa taratibu sisi tunatakiwa kuangalia wagombea uspika ambao sio wabunge kama wana sifa za kuwa wabunge, na tumepitia wasifu wa majina yote 23 tuliyoletewa na vyama na tumeona wana sifa za kuwa wabunge,” alisema Kailima na kuongeza: “Baada ya kukamilisha kwa upande wetu, tumeshamuandikia Katibu wa Bunge kutaka vyama viendelee na taratibu zao na kuwa wote wana sifa,” alisema.
Kailima alisema kati ya majina hayo 23, 17 walipelekwa na CCM, mmoja na Chadema, CHAUMMA ikitoa majina mawili, NRA, TLP na DP kila kimoja kimetoa mtu mmoja. Kwa mujibu wa Kanuni ya 9(4) ya Kanuni za Bunge inataka wagombea nafasi ya uspika wasio wabunge, vyama vinatakiwa kupeleka majina kwa NEC ili kuangalia kama watu hao wana sifa za kuwa wabunge. Imeandikwa na Amir Mhando, Dodoma na Anastazia Anyimike, Dar.