JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewabadilisha kazi wakaguzi saba na askari wa vyeo mbalimbali 157 wa Kikosi cha Usalama Barabarani ambao utendaji kazi wao umeonekana kukosa tija.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu, Suleiman Kova alisema uamuzi wa kuwabadilisha askari hao kutoka Kikosi cha Usalama Barabarani kwenda katika kazi za kawaida, umetokana na ufuatiliaji wa muda mrefu wa tabia na mwenendo wa askari hao wakati wa utendaji wa kazi.
“Utendaji wao umeonekana sio wa kuridhisha hadi umefikia kulalamikiwa na wananchi mara kwa mara hivyo kubadilishwa kwa askari ni hatua ya kwanza kwani bado uchunguzi zaidi unafanyika kwa wale wote watakaoendelea kufanya kazi chini ya kiwango,” alisema Kova.
Pia alisema askari ambao watabainika wamejihusisha na makosa ya moja kwa moja ya jinai kama vile kujihusisha na vitendo vya rushwa au ukiukwaji wa maadili ya Jeshi la Polisi watashitakiwa katika mahakama za kijeshi.
Alisema uchunguzi zaidi unaendelea kuhusu vikosi vingine vya Kanda Maalumu na Jeshi la Polisi kwa ujumla ili kubaini kama kuna askari, mkaguzi au ofisa anayefanya kazi chini ya kiwango kisichoridhisha na analalamikiwa.
Jeshi litachukua hatua kama hizo au nyingine kisheria. Aidha, Kova aliwataka watendaji wote wa Jeshi la Polisi kufanya kazi kwa bidii na weledi wa hali ya juu ili kuwahakikishia wananchi kwamba wananufaika kutokana na utendaji wa jeshi hilo na kulifanya Jiji la Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla pawe mahali salama pa kuishi.
Pia aliwataka wananchi na madereva kuacha kutengeneza mazingira ya rushwa ikiwemo kutengeneza makosa yanayosababisha rushwa. Katika tukio jingine, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imewakamata wahamiaji haramu 105 raia wa Ethiopia walioingia nchini bila kibali.
Akizungumzia tukio hilo, Kova alisema wahamiaji hao walikamatwa Tabata Segerea katika Manispaa ya Ilala baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasamaria. Alisema uchunguzi wa awali unaonesha watu hao walikuwa chini ya usimamizi wa mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Zabibu Umwiza (25) anayesemekana ni raia wa Burundi anayejihusisha na biashara ya usafirishaji wa binadamu kutoka nchi za Afrika kwenda Ulaya kwa malipo ya Dola za Marekani 1,000 (Sh milioni 1.2) kwa mtu mmoja.
|
0 Comments