UTARATIBU wa kuwazawadia wananchi wanaotoa taarifa za ukwepaji wa kodi umeokoa Sh 11,084,166,416 za kodi ambayo ilikusanywa baada ya wasamaria 62 kutoa taarifa za vitendo vya ukwepaji wa kodi.
Hii ni moja ya mipango madhubuti iliyobuniwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inayolenga kudhibiti ukwepaji kodi na kuongeza ukusanyaji wa mapato ya serikali. “Shabaha kubwa ya mkakati huu, ni kuwafanya wasamaria wema kufichua wakwepa kodi, na hakikisha Serikali inakusanya mapato zaidi yatakayosaidia kuharakisha maendeleo ya Watanzania,” alisema Mkurugenzi Idara ya Elimu na Huduma kwa Mlipakodi TRA, Richard Kayombo.

Chini ya mpango huo, wasamaria hao 62 wamefaidika kwa kuzawadiwa Sh 193,857,720 kwa taarifa (ambazo zimesaidia kuokoa mabilioni ya fedha) walizotoa kwa TRA katika kipindi cha mwaka 2014/2015. wasio waaminifu ambao kwa makusudi hukwepa kodi na kulipotezea taifa mapato,” alisema Kayombo.
Akifafanua, alisema TRA ilianzisha utaratibu wa kuwazawadia wananchi wanaotoa taarifa za ukwepaji wa kodi kwa kuwazawadia asilimia tatu ya kodi iliyookolewa ambapo kiasi cha zawadi kinatakiwa kisizidi milioni 20.
Katika mpango huu, taarifa za ukwepaji wa kodi zinazotolewa huchukuliwa kwa uzito wa hali ya juu na kufanyiwa uchunguzi wa kina ili kuhakikisha kwamba ni za ukweli na mtoa taarifa hubaki kuwa siri ya TRA.
Mamlaka ya Mapato imetoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa kuhusu vitendo vyovyote ambavyo vinasababisha mapato ya serikali kupotea ili kuweka uwiano sawa wa kila anayestahili kulipa kodi alipe kodi kwa mujibu wa sheria.
“Mwananchi yeyote mwenye taarifa za ukwepaji wa kodi anashauriwa kupiga simu namba 2137638 au 0784 210208 au anaweza kufika Mamlaka ya Mapato Tanzania Idara ya Uchunguzi wa Kodi. Baada ya hapo hatua stahiki zitachuliwa na mamlaka,” alisisitiza Kayombo.