BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), mpaka sasa imetoa mikopo kwa waombaji wenye sifa wapya 40,836 kati ya waombaji 50,830 wanaostahili kupatiwa mikopo hiyo kwa mwaka wa masomo wa 2015/2016.
Idadi hiyo imeongezeka baada ya Bodi hiyo jana kutoa awamu ya pili ya orodha yenye jumla ya waombaji 28,554 waliofanikiwa kupata mikopo hiyo katika mwaka huo wa masomo. Katika awamu ya kwanza, HESLB ilitoa orodha yenye jumla ya waombaji 12,282 waliopata mikopo hiyo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo, George Nyatega, hadi sasa imekwishawapangia mikopo jumla ya waombaji mikopo wenye sifa 40,836 wa mwaka wa kwanza kwa mwaka wa masomo 2015/2016. “Majina ya waombaji waliofanikiwa kupata mikopo kutoka katika awamu zote mbili yanapatikana kupitia mtandao wa Bodi wa olas.heslb. go.tz na tovuti ya Bodi (www.heslb. go.tz),” alisema Nyatega.
Aidha, alisema orodha hizo pia zimetumwa vyuoni kwa ajili ya taratibu za usajili. Alisema lengo la Bodi hiyo ni kuhakikisha kuwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza wenye sifa ya kupata mikopo katika mwaka wa masomo 2015/2016 ambao ni 50,830, wote wanapata mikopo.
“Bodi inapenda kuwasihi waombaji wa mikopo kuwa watulivu wakati mchakato wa upangaji wa mikopo kwa wanafunzi wenye sifa unaendelea,” alisisitiza Nyatega. Mwaka wa masomo wa 2014/2015, Bodi hiyo ilitoa mikopo kwa wanafunzi wapya takribani 33,000.
Aidha, Nyatega aliwataka Watanzania kupuuza taarifa zisizo za kweli zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba, HESLB, haitatoa mikopo kwa waombaji wapya. Hivi karibuni, baada ya Bodi hiyo kutoa orodha ya waombaji wa awamu ya kwanza waliofanikiwa kupata mikopo hiyo, Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) lilitoa saa 72 kwa bodi hiyo iwe imetoa ufafanuzi juu ya vigezo vilivyotumika kuwapatia wanafunzi hao wachache mikopo.
Aidha, katika baadhi ya mitandao ya kijamii zilienezwa taarifa zinazodai kuwa bodi hiyo, mwaka huu wa masomo 2015/2016, imetoa mikopo kwa waombaji asilimia 18 pekee huku baadhi ya vyuo vikitajwa kukosa hata mwanafunzi mmoja aliyepatiwa mikopo hiyo.
Kutokana na malalamiko na madai kwamba huenda takribani asilimia 82 ya wanafunzi walioomba kupatiwa mikopo wakakosa mikopo hiyo, Rais Dk John Magufuli alipokutana na makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu na watendaji wakuu wa Serikali, aliagiza suala hilo lishughulikiwe haraka iwezekanavyo. Dk Magufuli aliagiza suala la mikopo ya wanafunzi lifanyiwe kazi haraka na mipango yake ikamilike kwa ajili ya utekelezaji mzuri zaidi.