KATIKA kutekeleza mpango wa utoaji elimu bure kwa shule za serikali za msingi na sekondari nchini, Serikali itapeleka moja kwa moja shuleni kutoka Hazina wastani wa Sh bilioni 18.77 kwa kila mwezi.
Kwa kuanzia serikali imetenga jumla ya Sh bilioni 131.4 ikiwa ni fedha za ruzuku za uendeshaji wa shule, chakula, mitihani na fidia ya ada. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene alisema jana katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini hapa na kubainisha kuwa tayari baadhi ya shule zimeanza kupokea fedha za ruzuku kwa ajili ya kuanza muhula wa masomo mapema wiki ijayo.

Alisema Serikali italipa ruzuku za uendeshaji wa shule za msingi na sekondari, ikiwa ni pamoja na wanafunzi wa bweni kupatiwa chakula bila gharama yoyote, huku gharama za mitihani ya kidato cha nne zitalipwa moja kwa moja kwenye Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA). Alisema fedha hizo ni kwa ajili ya ruzuku ya uendeshaji wa shule ya Sh 10,000 kwa mwanafunzi wa shule ya msingi na Sh 25,000 kwa mwanafunzi wa sekondari kwa mwaka.
Pia Sh 1,500 kwa siku kwa mwanafunzi wa shule za msingi na sekondari kwa ajili ya chakula kwa wanafunzi wanaokaa shule za bweni. Alisema fidia ya ada ya Sh 20,000 kwa mwanafunzi wa kutwa na Sh 70,000 kwa mwanafunzi wa bweni wa kidato cha kwanza hadi cha nne kila mwaka. Alisema gharama za mitihani ya kidato cha nne, zitalipwa na serikali moja kwa moja NECTA, hivyo wazazi au walezi hawatagharamia fedha hizo tena.
Waziri huyo alisema wazazi na walezi watawajibika katika kununua sare za shule na michezo, vifaa vya kujifunzia vikiwemo madaftari na kalamu, chakula kwa wanafunzi wa kutwa. Pia kugharamia matibabu ya watoto wao, kulipa nauli ya kwenda na kurudi shuleni kwa wanafunzi wa kutwa na wa bweni wakati wa likizo, kununua magodoro, shuka na vifaa vya usafi.
Aidha aliwataka wazazi na walezi kukemea na kutoa taarifa kwenye mamlaka za serikali zilizo karibu nao kuhusu mienendo inayokwenda kinyume na elimu bila malipo. Alitoa mwito kwa viongozi wote wakiwemo wakuu wa mikoa, wilaya, makatibu tawala wa mikoa, wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa kusimamia utekelezaji wa elimu bila malipo.
Alisema jamii inayozunguka shule itaendelea na wajibu katika utoaji wa elimu ya msingi bila malipo kwa kujitolea pale itakapokuwa imekubalika nguvukazi na mali ili kuleta ustawi na maendeleo ya shule katika jamii husika Pia kuhamasisha wazazi na walezi wenye watoto wa umri wa kwenda shule, kuwapeleka shule na wabaki shuleni wakati wote wa masomo ili wapate elimu.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari, waliotaka kufahamu madai mbalimbali ya fedha za wazabuni wanaosambaza chakula kwenye shule za bweni kama yatalipwa kutokana na fedha hizo, Waziri Simbachawene alisema hawapeleki fedha shuleni kwa ajili ya kulipa madeni, lakini madeni hayo yatalipwa baada ya michakato yake kukamilika.
Aliwataka walimu wakuu na wakuu wa shule, kutumia fedha hizo kama zilivyokusudiwa na hatua kali zitachukuliwa, iwapo kutakuwa na wizi au fedha kutumika kwa matumizi mengine. Alisema fedha ambazo zitapelekwa mashuleni ni zile zilizotokana na makusanyo ya wakwepa kodi.
“Rais amefanya maamuzi ya busara fedha hii ingetakiwa kupitishwa kwenye bajeti ndio iende kwenye elimu lakini ameona umuhimu wa wananchi kupata elimu bila kujali mwenye nacho na asiye nacho,” alisema.