Guus-Hiddink

Ikiwa zimepita siku tatu tangu uongozi wa klabu ya Chelsea kumtimua kazi aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Mreno Jose Mourinho hatimaye taarifa zimetoka ndani ya timu hiyo kuwa, Mholanzi Guus Hiddink (pichani) amekuwa meneja mpya wa klabu hiyo ya Uingereza.
Katika taarifa iliyotolewa na ukurasa wa klabu hiyo wa Twitter umeeleza kuwa Hiddink atakuwa meneja wa Chelsea mpaka mwisho wa msimu huu wa 2015/2016.

Hiddink hii siyo mara yake ya kwanza kuifundisha timu hiyo ya London, aliwahi kuifundisha kwa kipindi kifupi mwaka 2009 na kuisaidia timu hiyo kutwaa taji la Kombe la FA na kumaliza nafasi ya pili katika Ligi Kuu ya Uingereza nyuma ya Manchester United.
Baada ya taarifa kutoka, Hiddink amezungumza na mtandao wa Chelsea na kusema kuwa ni jambo la furaha kurejea tena kuifundisha timu hiyo na anatambua kuwa hiyo ni timu kubwa hivyo atajitahidi kadri ya uwezo wake kujaribu kuweka mambo sawa ili kuwapa furaha mashabiki wa timu hiyo.
“Nimefurahishwa na kurudi tena darajani, Chelsea ni moja ya timu kubwa duniani na haipaswi kuwa katika hali iliyonayo sasa, nina amini tutaweka kila jambo sawa kama lilivyokuwa,
“Ninachokiangalia kwa sasa ni kufanya kazi na wachezaji na uongozi katika hii klabu kubwa na kitu kizuri narudi katika timu ambayo ina mashabiki wanaojua kushangilia timu yao,” alisema Hiddink.
Mpaka sasa Chelsea wameshakusanya alama 18 katika michezo 17 ya Ligi Kuu ya Uingereza ambayo wameshacheza kwa msimu huu na mchezo wa kwanza wa Hiddink unatarajiwa kuwa dhidi ya Watford, Disemba 26 siku ya Kufugua Zawadi “Boxing-Day”
Na Rabi Hume, Modewjiblog