JAJI wa Mahakama Kuu, Jaji Gadi Mjemas anayesikiliza kesi ya kughushi nyaraka na kutakatisha fedha inayomkabili Wakili maarufu Median Mwale na wenzake watatu, amemtaka Wakili wa Serikali, Pius Hilla kumwelekeza shahidi wa kesi hiyo kitu gani alichunguza badala ya kumuuliza kozi alizohudhuria kwani zinapoteza muda.
Jaji Mjemas aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati alipomuingilia kati wakili Hilla aliyekuwa akimwongoza shahidi Suleiman Nyakulinga (49) ambaye ni Ofisa wa Polisi kutoka Makao Makuu ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai kutoa ushahidi wake mahakamani hapo.
Wakili Hilla wakati akimuongoza Nyakulinga alimtaka kueleza mafunzo mbalimbali ya upelelezi aliyohudhuria ndani na nje ya nchi.
“Aaah.. wakili unahoji mafunzo aliyoyapata kwani unataka kumwajiri hebu nenda katika pointi muhimu ambayo imemleta hapa lengo ni kuisaidia mahakama na si vinginevyo tafadhali”.
Baada ya kauli ya Jaji Mjemas wakili Hilla alirudi katika mstari na kumwezesha Nyakulinga kuusema ushahidi wake.
Alisema baada ya kukabidhiwa kazi ya uchunguzi katika Benki ya CRDB tawi la Meru Jijini Arusha, alifuatilia taarifa mbalimbali katika benki hiyo na kufanya mahojiano na Meneja wa benki ambaye kwa sasa ni mshitakiwa, Boniface Mwimbwa ili kujua kama kweli akaunti za Moyale Precious Gems Mineral and Enterprise Ltd na Taasisi ya Kimataifa ya Global Fund na ambayo iliingiza fedha za kimarekani katika akaunti yao ya East African and Malaria and HIV and Support Program, iliyopo tawi la Meru katika Benki ya CRDB Arusha zilifunguliwa kihalali au la.
Na baada ya kupewa nyaraka mbalimbali na kuzichunguza yeye na ASP Fadhil Mdemu waligundua kuwa akaunti ya kampuni ya Moyale ilifunguliwa na watu wawili ambao ni Mitchel Ogembo Chacha na Gregg Mutachwa Mwita ambao walikuwa na vitambulisho vya makazi ambazo zinafanana na pia hati zao za kusafiria zinafanana.
Mara baada ya Nyakulinga kueleza jinsi alivyochunguza kesi hiyo aliomba nyaraka mbalimbali kupokewa kama ushahidi wa vielelezo mahakamani hapo lakini upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Omary Omary na mawakili wenzake Innocent Mwanga, Albert Msando, Julieth Tarimo, Mosses Mahuna Buheri Ngoseki ulipinga baadhi ya nyaraka hizo.
Wakili Median Mwale na wenzake Don Bosco Gichana (Raia wa Kenya) Boniface Mwimbwa na Elias Ndejembi ambao wanakabiliwa na mashitaka 42 tofauti tofauti, ikiwemo la utakatishaji fedha haramu, kughushi nyaraka na kukutwa na mali zilizopatikana kwa njia za uhalifu.
|
0 Comments