RAIS John Magufuli ameendelea kuthibitisha kuwa hana mchezo katika usimamizi wa mali za umma, baada ya jana kumsimamisha kigogo mwingine katika mashirika ya umma kutokana na ubadhirifu na kuvunja Bodi mbili.
Dk Magufuli amemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (RAHCO), Benhadard Tito ili kupisha uchunguzi wa kina kutokana na ukiukwaji mkubwa wa taratibu za manunuzi, uliobainika katika mchakato wa utoaji wa zabuni ya ujenzi wa Reli ya Kati.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue, Dk Magufuli amefikia uamuzi huo baada ya kuitisha kikao cha wataalamu kutoka wizara na taasisi mbalimbali za serikali, ambazo zinahusika katika utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kisasa yaani “standard gauge.”
Balozi Sefue alisema pamoja na kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Rahco, Rais Magufuli ameivunja Bodi ya Rahco baada ya kujiridhisha kuwa haikutekeleza ipasavyo wajibu wake katika kusimamia mchakato wa zabuni hiyo na badala yake imeonekana kutetea kilichofanyika.
Aidha, Rais Magufuli amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa Rahco, Tito ambaye kitaaluma ni Mhandisi, kutoa ushirikiano kwa vyombo vya serikali vitakavyofanya uchunguzi zaidi kuhusu mchakato wa zabuni hiyo.
Pia ameiagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kuchunguza na kuchukua hatua dhidi ya kampuni za ukandarasi zilizopewa zabuni ya ujenzi huo, endapo itathibitika zilishiriki katika ukiukwaji wa sheria.
Katika hatua nyingine, Balozi Sefue alisema Dk Magufuli amevunja Bodi ya Mamlaka ya Reli Tanzania (TRL) kutokana na kutoridhishwa na jinsi ilivyoshughulikia ripoti ya uchunguzi wa mchakato wa ununuzi wa mabehewa ya treni.
Kwa mujibu wa tovuti ya TRL, Bodi yake ilikuwa ikiongozwa na Mwenyekiti aliyetajwa kwa jina moja la Kaombwe, na wajumbe wake ni Vincent Mrisho, Malima Bundara, aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji Kipalo Kisamfu, na wawili waliotajwa kwa jina moja moja la Shamte na Kipande.
Bodi ya Wakurugenzi ya Rahco ilikuwa ikiongozwa na Profesa Mwanuzi Fredrick na baadhi ya wajumbe wake ni Stella Manongi, Suleiman Suleiman na Gideon Nassari.
Ilizinduliwa Oktoba 29, mwaka huu, na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk Shaaban Mwinjaka ambaye uteuzi wake ulitenguliwa na Rais Magufuli hivi karibuni kwa kushindwa kusimamia utendaji wa TRL na TPA.
Aprili mwaka huu, aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta aliwasimamisha kazi viongozi wakuu watano wa TRL kutokana na kuingizwa na kulipwa kwa manunuzi ya mabehewa mabovu, ili kupisha uchunguzi.
Viongozi hao ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Reli, Kipalo Kisamfu; Mhandisi Mkuu wa Mitambo, Ngosomwile Ngosomiles; Mhasibu Mkuu wa Kampuni, Mbaraka Mchopa; Mkaguzi Mkuu wa Ndani, Jasper Kisiraga na Meneja Mkuu wa Manunuzi, Ferdinand Soka.
Kusimamishwa kwa Tito na kuvunjwa kwa Bodi za Rahco na TRL ni mwendelezo wa hatua anazochukua Rais Magufuli katika kukabiliana na ufisadi katika kile ambacho mwenyewe alikipachika jina la ‘kutumbua majipu.’
Mbali ya kutengua uteuzi wa Dk Mwinjaka, Rais ameshavunja Bodi ya Mamlaka ya Bandari (TPA) na kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Bandari, Awadh Massawe.
Aidha, amemsimamisha Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade kutokana na ubadhirifu wa mapato katika Bandari ya Dar es Salaam, pamoja na kusimamishwa kwa maofisa wengine wa TPA na wale wa TRA, ambao baadhi yao wamepandishwa kizimbani.
Hivi karibuni, Rais Magufuli pia alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah kutokana na ulegelege wa taasisi hiyo katika kukabili rushwa, hasa suala la upotevu wa mapato bandarini kupitia sakata la makontena takribani 3,000.
Wakati huo huo, pamoja na kusimamishwa kazi kwa Mkurugenzi Mkuu wa RAHCO, Mhandisi Tito na kuvunjwa kwa Bodi ya RAHCO, Rais Magufuli pia amemuagiza Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Valentino Mlowola, kuanza uchunguzi wa kina mara moja kuhusu sakata hilo la ukiukwaji wa sheria ya manunuzi katika zabuni ya ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kisasa, yaani “standard gauge”.
|
0 Comments