WAZIRI wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk Augustine Mahiga amesema Tanzania iko mstari wa mbele kushughulikia mgogoro unaoendelea nchini Burundi.
Balozi Mahiga alisema sio kweli kuwa Tanzania imekaa kimya na haijishughulishi na mgogoro huo, bali ilikuwa imekasimu kazi hiyo kwa Serikali ya Uganda kutokana na majukumu mazito yaliyokuwa yakiikabili nchi hususan Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba mwaka huu.

Alitoa kauli hiyo juzi alipozungumza na vyombo vya habari Arusha wakati wa ziara ya kujitambulisha kwa Bodi mpya ya Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) na kutembelea miradi mbalimbali ya kituo hicho.
Alisema Tanzania kutokana na kukabiliwa na mambo mbalimbali likiwemo la uchaguzi, kuchelewa kutangazwa kwa Baraza la Mawaziri ndipo ilipoamua kukasimu uongozi wake wa Uenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa Uganda ili kuanzisha mazungumzo kuhusu mgogoro huo.
Aliongeza kuwa baada ya Tanzania kuwa katika hali nzuri ya kujikita katika kutafuta suluhu ya mgogoro huo, ndipo yeye kama waziri wa masuala hayo, alipopokea maagizo kutoka kwa Rais John Magufuli ya kutakiwa kufanya maandalizi yote kwa ajili ya kuanza kwa mazungumzo hayo.
Alisema tayari ameshaanza mchakato wa kukutana na mawaziri wenzake wa Mambo ya Nje wa EAC ili kukubaliana mambo watakayoyawasilisha kwa viongozi wakuu wa nchi zao ili nao wakutane kwa ajili hiyo.
Alisema kamwe Tanzania haifurahishwi na hali inayoendelea Burundi,kwa kuwa ndiyo hasa nchi inayoathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na hali hiyo, kutokana na kupokea wakimbizi wengi wanaotoka nchini humo.
Alisema mbali na upokeaji wa wakimbizi wengi waliofikia zaidi ya 2,000, pia Tanzania imekuwa ikipata madhara ya kuingia kwa silaha za kivita kupitia wakimbizi hao, na hivyo kujikuta zikiwa zinatumika katika uhalifu.
Aidha, alisema kutokana na ukweli huo ndipo ambapo Rais Magufuli akiwa kama Mwenyekiti wa EAC, alipoamua kuchukua hatua mbalimbali za mazungumzo na marais wenzake wa jumuiya akiwemo Uhuru Kenyatta wa Kenya, Yoweri Museveni wa Uganda pamoja na Paul Kagame wa Rwanda katika kutafuta suluhu ya mgogoro huo.
Aidha, jana mchana Balozi Mahiga alitarajiwa kukutana na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Richard Sezibera mjini hapa, kujadili pamoja na mambo mengine, suala la Burundi lilitarajiwa kujadiliwa.