WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa anatarajia kuanza ziara ya kiserikali ya siku mbili mkoani Kigoma kuanzia leo ikiwa ni ziara yake ya kwanza mkoani hapa tangu alipochaguliwa kuwa Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu Majaliwa ambaye anatarajia kuwasili saa 3:00 asubuhi katika Uwanja wa Ndege wa Kigoma, anatarajia kupokewa na viongozi mbalimbali wa serikali na wananchi wa mkoa huo wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Kigoma, Issa Machibya.
Katika taarifa yake kwa waandishi wa habari Mkuu wa Mkoa Kigoma, Machibya alisema kuwa atakapowasili mkoani Kigoma katika siku yake ya kwanza, Waziri Mkuu atasomewa taarifa ya utendaji wa shughuli za serikali mkoani humo.
Machibya alisema baada ya taarifa hiyo Waziri Mkuu ataelekea wilayani Kasulu ambapo atatembelea kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu ambayo kwa sasa inahifadhi wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Burundi.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa baadaye Waziri Mkuu Majaliwa ataelekea kambi ya wakimbizi ya Nduta wilayani Kibondo ambapo wanahamishiwa wakimbizi wa Burundi wanaohifadhiwa kwenye kambi na atamaliza ziara yake kwa siku ya kwanza kwa kurejea mjini Kigoma.
Aidha Machibya alisema katika siku yake ya pili ya ziara yake mkoani Kigoma Waziri Mkuu atafungua Soko la Kimataifa la Samaki katika Bandari ndogo ya Kibirizi mjini Kigoma lililojengwa kwa Ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).
Baadaye atakuwa na mkutano wa majumuisho wa ziara yake mkoani Kigoma kwa kukutana na viongozi wa mkoa, halmashauri, taasisi na mashirika ya serikali yanayofanya shughuli zake mkoani Kigoma ambapo baada ya mkutano huo atarejea Dar es Salaam.
|
0 Comments