SERIKALI imepiga marufuku matangazo yote ya tiba asili na tiba mbadala katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuanzia jana. Aidha, wale wote wenye vibali wanatakiwa kuwasilisha vibali na matangazo hivyo katika Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala kwa ajili ya kuvifanyia mapitio upya.
Amri hiyo imetolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ikiwa ni matokeo baada ya ziara ya Naibu Waziri wa wizara hiyo, Dk Hamis Kingwangala aliyoifanya katika kliniki ya tabibu Dk Mwaka Desemba 14 mwaka huu.
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Michael John alisema katika taarifa yake kwa umma kuwa licha ya kuwa utoaji huduma hiyo ya tiba asili kuwa na historia ndefu nchini, lakini imebainika kuwepo kwa mapungufu kadhaa.
“Matangazo yote yanayohusu tiba asilia na Tiba mbadala kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, yanapigwa marufuku mara moja kwa wale wenye vibali wanatakiwa wawasilishe vibali na matangazo yao kwenye Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala vifanyiwe uhakiki,” alisema taarifa hiyo ya John.
Aidha, utoaji wa elimu ya afya kwa umma unaofanywa na watoa huduma za tiba asilia na tiba mbadala kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, nao umepigwa marufuku hadi hapo utaratibu mwingine utakapotolewa.
Watoa huduma wa Tiba asili na Tiba Mbadala nchini kote, wamepewa siku 14 wawe wamewasilisha kwa baraza nyaraka zote muhimu, ikiwa ni pamoja na nyaraka za kuuza dawa za asili na tiba mbadala na nyaraka za kumiliki mashine zinazotumika katika kufanya uchunguzi katika tiba asilia na tiba mbadala.
Wizara pia imelitaka Baraza la Tiba asili na Tiba mbadala katika kipindi cha siku 14 kuanzia jana, kupitia nyaraka zote zitakazowasilishwa zinazohusu usajili wa watoa huduma, usajili wa vituo na maduka ya dawa asilia na dawa za tiba mbadala na mashine zinazotumika katika huduma za tiba asilia na tiba mbadala.
|
0 Comments