MKULIMA mmoja ameuawa kwa kuchomwa na mkuki na zaidi ya ng’ombe 71 wameuawa kwa kukatwakatwa mapanga wakati wa mapigano ya wakulima na wafugaji, yaliyotokea katika Kijiji cha Dihinda katika Kata ya Kanga Wilaya ya Mvomero Mkoa wa Morogoro.
Aidha, katika tukio hilo lililotokea Desemba 12, watu wanne akiwemo askari mmoja wa Jeshi la Polisi walijeruhiwa na wamelazwa katika Hospitali ya Misheni ya Bwagala mjini Turiani wakiendelea kupatiwa matibabu.
Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Rajabu Kilama alisema mapigano hayo yalitokea baada ya ng’ombe 162 kuingia katika shamba la kunde la Bakari Mlunguza na kuharibu zao hilo.
Mwenyekiti huyo alisema baadaye ng’ombe hao, ambao ni mali ya Shabani Mang’ati ambaye ni mfugaji wa jamii ya Kibarbaig, walikamatwa na kuzuiwa kwa lengo la kumpata mfugaji huyo ili alipe faini ambayo ni Sh 200,000.
Alisema baada ya kupatikana, mfugaji huyo alikubali kulipa faini hiyo na kuomba apewe muda wa kwenda kuchukua fedha, lakini muda mfupi kundi la wafugaji wenzake wakiwa na silaha walianza kuwashambulia watu waliokuwa wakilinda ng’ombe hao na kumuua mkulima mmoja.
Kilama alisema kutokana na mauaji hayo, wakulima nao walijikusanya na kuanza kukatakata ng’ombe kwa mapanga, hali iliyosababisha ng’ombe 71 kufa na wengine zaidi ya 80 kujeruhiwa.
Mmoja wa wananchi wa kijiji hicho, Ally Mkwaya alisema kwa sasa hofu imetanda kijijini hapo, hali iliyosababisha baadhi yao kuhama makazi na familia zao na kukimbilia vijiji vya jirani wakihofia kuuawa.
“Mimi nimehamisha mke wangu na watoto kwenda kijiji cha jirani na kwa sasa nimekuwa sina amani na nashindwa hata kwenda shamba kwa sababu wafugaji wamekuwa wakivizia wakulima mashambani na wanatumia silaha,” alisema Mkwaya.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Betty Mkwasa alisema mapigano hayo, yamekuja wakati Serikali ya Wilaya hiyo ikijipanga kufanya operesheni ya kuwaondoa wafugaji wavamizi kwani kwa asilimia kubwa kijiji hicho ni cha wakulima.
Mkwasa alisema mifugo inayoingia katika kijiji hicho ni ile inay oondolewa katika Hifadhi ya Wami Mbiki na mingine inayotokea wilaya za Handeni, Kilindi mkoani Tanga na Manyara, hivyo imekuwa ikiingia katika vijiji vya wakulima na kusababisha migogoro.
Naye Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba alilaani mauaji ya mkulima pamoja na mifugo, ambayo haikuwa na hatia yoyote, na kumuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo kuhakikisha wote waliohusika katika tukio hilo, wanakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Pia ameonya uuzaji holela wa ardhi, kwani alisema unasababisha uvamizi katika maeneo ya wakulima na wafugaji na kuacha tabia ya kujichukulia sheria mikononi, badala yake waende kwenye vyombo vyenye mamlaka ya kutoa maamuzi.
Baada ya msako mkali, Polisi imewakata watu watatu kwa tuhuma za kuhusika kuua ng’ombe na watu 16 kwa tuhuma za mauaji ya mkulima. Aidha, limeimarisha ulinzi katika kijiji hicho na vijiji vya jirani ili kuhakikisha hali ya usalama inarejea.
|
0 Comments