WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amewaomba Watanzania kuendelea kumuombea Rais John Magufuli, kwani kazi ya kutumbua majipu ambayo ameianza ni kazi ngumu na yenye vikwazo.
Sambamba na hilo, amewataka Watanzania na waumini wa madhehebu yote nchini, kuwaombea pia wasaidizi wa Rais ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa kwa lengo la kuleta tija kwa Watanzania wote.
Akizungumza juzi jijini Dar es Salaam kwenye uzinduzi wa albamu mbili za kwaya ya Wakorintho wa Pili katika tamasha la Krismasi, ambapo alikuwa mgeni rasmi akimwakilisha Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan, Nape alisema kazi ya kutumbua majipu sio rahisi.
“Watanzania wenzangu kila mmoja kwa dhehebu lake, tuendelee kumuombea rais wetu, kazi ya kutumbua majipu sio rahisi, ina vikwazo vingi”, alisema Nape. Katika tamasha hilo, mwimbaji wa muziki wa Injili kutoka Afrika ya Kusini, Rebecca Malope alifanya onesho kubwa akishirikiana na waimbaji mbalimbali wa hapa nchini na nchi jirani ya Kenya, ambapo lilivuta hisia za mashabiki wengi waliohudhuria.
Nape alisisitiza kuwa ili rasilimali za nchi ziwanufaishe wote, ni vyema kumuunga mkono Rais Magufuli kwa kuwaombea pia wasaidizi wake ili wafanye kazi kwa kasi atakayo Rais na yenye kiwango.
Katika tamasha hilo, waimbaji wengine waliokuwepo ni pamoja na Faustine Munishi, Sara K, Solomon Mukubwa kutoka Kenya. Wengine wa hapa nchini ni Rose Mhando, Upendo Nkone, Christine Shusho, Edson Mwasabwite, Joshua Mlelwa na wengine . Tamasha hilo pia lilikuwa na lengo la kumshukuru Mungu kwa nchi kufanya uchaguzi kwa amani.
|
0 Comments