MFANYAKAZI wa bustani, Ismail Swalehe Sang’wa (20), mkazi wa kijiji cha Sepuka wilayani Ikungi mkoa wa Singida, amekamatwa na Polisi, akituhumiwa kumchinja Kachero wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), Emily Stephano Kisamo (52).
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas aliwaambia waandishi wa habari kwamba, mtuhumiwa huyo alikuwa mfanyakazi wa bustani nyumbani kwa Kisamo. Aidha, Polisi inamshikilia mke wa marehemu, Caroline Lukumay (38) na rafiki yake wa kike (ambaye hakutajwa jina) na dereva aliyekuwa akitumiwa na Kisamo kwa shughuli za nyumbani na si ofisini.
Kamanda alidai mfanyakazi huyo wa bustani alipokamatwa na Polisi, alikiri kumchinja shingoni kwa kutumia panga; baada ya kumvizia akiwa anakunywa uji sebuleni, nyumbani kwake eneo la Corridor Area Uzunguni, Desemba 18 mwaka huu .
Kwa mujibu wa kamanda, katika mahojiano na kijana huyo, alikiri kumuua ‘bosi’ wake apate Sh milioni tano alizokuwa nazo wakati akijiandaa na safari ya kwenda India kesho yake kwenye matibabu.
“Tulipomkamata alikiri na kutuonesha panga alilotumia kumchinja marehemu likiwa na damu amelificha stoo, fedha hizo alikoficha ambazo shilingi 4,294,000, simu tatu za Sumsung, nguo alizofutia damu na vocha aina ya Vodacom za 5,000 zenye thamani ya Sh 70,000 vyote hivyo vilikuwa vimefunikwa kwenye banda la kuku,” alisema Kamanda.
Kamanda Sabas alisema pia mtuhumiwa aliwaonesha polisi taulo kubwa nne zikiwa na damu, kitambaa cha mezani, suruali moja ya mtuhumiwa ambazo zilifichwa kwenye migomba karibu na mabanda ya kuku na zilikuwa na damu, ambavyo vyote mtuhumiwa alidai alivitumia kupiga navyo deki kuondoa damu.
Alisema baada ya kumaliza kumchinja shingo, alifanya usafi kwa kupiga deki eneo alilofanya mauaji hayo na kisha kusafisha gari kwa nje, kisha kumweka kwenye buti la gari lake lenye namba T. 435 CSY aina ya Nissan Mazda na kuliendesha mpaka eneo la Likwakwaru na kulitelekeza.
Akizungumzia mke wa marehemu, Kamanda alisema anaendelea kushikiliwa pamoja na watuhumiwa wengine, kupata taarifa zaidi za kifo hicho kwa ajili ya kuchukua hatua. Mwili wa kachero huyo, ulipatikana kwenye gari lake Desemba 19 mwaka huu.
Baada ya gari kukutwa limetelekezwa, polisi walilifunga minyororo na kulivuta hadi kituo cha Polisi na kumwomba funguo wa gari wa akiba mke wa marehemu. Polisi walipofungua walikuta mwili ndani ya buti ukiwa umechinjwa shingoni.
Awali mke huyo alitoa taarifa kuwa mumewe amepotea nyumbani Desemba 18 na kwamba akimpigia, simu zake zilikuwa zikiita bila kupokewa. Kamanda wa Polisi aliwaambia waandishi kwamba awali kuuawa kwa kachero huyo, kulihisiwa na kazi alizokuwa akizifanya; lakini wamebaini kuwa hakuna uhusiano wowote na kazi bali ni tamaa ya mali.
Kwa mujibu wa ndugu wa marehemu, maziko yake yanatarajiwa kufanyika Marangu mkoani Kilimanjaro.
|
0 Comments