ASASI za Kiraia nchini (Azaki) zimepongeza hali ya amani iliyoko visiwani Zanzibar tangu kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka jana hadi sasa. Tamko hilo la Azaki kuhusu hali ya kisiasa visiwani Zanzibar, lilisomwa jana jijini Dar es Salaam na Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa.
Viongozi wengine wa asasi walioshiriki mkutano na tamko hilo ni Katibu Mkuu Baraza la Asasi za Kiraia (Nacongo) na Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Martina Kabisama.
Wengine ni Stephen Msechu wa Mtandao wa Mashirika ya Haki za Binadamu Kusini mwa Afrika (Sahringon), Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Omary Said; Mwakilishi wa Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS), Salma Said na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (Wahamaza).
Asasi hizo zilipongeza wananchi na wanasiasa kwa kudumisha amani na kutoleta machafuko visiwani humo. Olengurumwa alisema: “Tunawapongeza wananchi na wanasiasa wote wa Zanzibar kwa kudumisha amani na utulivu katika kipindi chote tangu kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Oktoba mwaka jana”.
Olengurumwa alisema muungano huo wa asasi za kiraia, unatambua hatua za busara za viongozi kutambua wajibu wao na kukutana kujadili njia ya kuondoa mgogoro uliopo wa kiuongozi. Aliwataka viongozi wanaokutana katika majadiliano, kuweka hadharani hatma ya mazungumzo yao.
“Viongozi wamepata muda wa kutosha kwa viongozi wanaokutana kutoka hadharani, ikiwezekana siku ya maadhimisho ya Mapinduzi ya Zanzibar, tena kwa pamoja na kutoa taarifa ya ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya mazungumzo,”alisema Olengurumwa.
Azaki hizo zilitoa mwito kwa viongozi wa serikali, kutumia siku ya Mapinduzi kuwatangazia wananchi hatma ya Zanzibar kisiasa, kwa kuwa wananchi wanayo haki na uhuru wa kushiriki kwa ukamilifu katika uamuzi wa mambo yao na taifa. Olengurumwa pia alivikumbusha vyama vya siasa nchini, kushinikiza serikali ya Awamu ya Tano, kupatia ufumbuzi mgogoro huo wa kisiasa Zanzibar ili wananchi waendelee na shughuli zao za maendeleo.
Alitaka pande zote zinazohusika katika mgogoro huo, kujiepusha kutoa kauli za kuwachanganya wananchi. Alitaka taarifa zinazotolewa, ziwe sahihi na zisiwe na mkanganyiko. Tangazo la ZEC Oktoba 28 mwaka jana, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, alitoa “Taarifa Kwa Umma ya Kufuta Uchaguzi wa Zanzibar”.
Katika taarifa hiyo, Jecha Salim Jecha alisema “Mimi nikiwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, nimeridhika kwamba uchaguzi huu haukuwa wa haki na kuna ukiukwaji mkubwa wa Sheria na taratibu za uchaguzi. Hivyo, kwa uwezo nilionao natangaza rasmi kwamba uchaguzi huu na matokeo yake yote yamefutwa na kwamba kuna haja ya kurudia uchaguzi huu”.
Alisema ZEC imefanya utafiti na kujiridhisha na hatimaye kuamua kufuta matokeo yote ya uchaguzi huo ili urudiwe. Jecha alitaja sababu zilizosababisha kufutwa kwa uchaguzi huo wa Zanzibar kuwa ni: Baadhi ya vituo vya uchaguzi katika Kisiwa cha Pemba kuwa na idadi kubwa ya kura, zilizopigwa kuliko idadi ya watu waliopo katika Daftari la Wapiga Kura. Sababu nyingine ni kadi za kupigia kura hazijachukuliwa, lakini watu wamepiga kura.
Jecha alisema sababu nyingine ni kuvamiwa kwa vituo vya kupigia kura na kuibuka kwa fujo na kusababisha watu wengine kushindwa kupiga kura. Fujo katika vituo vya kupigia kura zilijitokeza katika majimbo yaliyopo kisiwa cha Pemba, ikiwemo Micheweni, Tumbe na Konde.
Alitaja sababu nyingine ni vyama vya siasa kuingilia mchakato na kazi za Tume ya Uchaguzi na hatimaye baadhi ya vyama, kujitangazia ushindi katika uchaguzi huo, ikiwa ni kinyume cha sheria za Tume ya Uchaguzi. Alisema uamuzi wa kutangaza matokeo ya urais kinyume cha sheria za Tume ya Uchaguzi ni hatari na ungeweza kuliingiza taifa katika machafuko.
“Hizo ndiyo sababu ambazo zimepelekea uchaguzi wote ulio fanyika Oktoba 25 kufutwa matokeo yake,” alisema Jecha wakati akitoa taarifa hiyo katika Televisheni ya Zanzibar (ZBC). Hata hivyo, hakutaja lini na tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi mwingine.
Katiba ya Zanzibar inasemaje? Kifungu Namba 28 (i) (a) cha Katiba ya Zanzibar Toleo la mwaka 2010, kinasema kuwa “ Mtu ataendelea na kuwa Rais mpaka rais anayefuata ale kiapo cha kuwa Rais”.
Pia Kifungu Namba 119 (12) cha Katiba hiyo ya Zanzibar, kinasema “katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya katiba, Tume ya Uchaguzi haitalazimika kufuata amri au maagizo ya mtu yeyote au idara yoyote ya serikali, au maoni ya chama cha siasa”.
|
0 Comments