Polisi mjini Munich wamefunga vituo vikuu viwili vya treni baada ya idara ya ujasusi kuonya kuwa kungetokea shambulio, maafisa wanasema.
Maafisa wa usalama walipokea habari kwamba washambuliaji wa kujitoa mhanga kutoka kundi linalojiita Islamic State (IS) wangeshambulio kituo kikuu cha magari moshi au kituo cha Pasing, kwa mujibu wa waziri wa masuaa ya ndani wa Bavaria.

Vituo hivyo baadaye vimefunguliwa, polisi wameandika kwenye Twitter.
Miji mbalimbali Ulaya imekuwa kwenye hali ya juu ya tahadhari kutokana na wasiwasi wa kutekelezwa kwa mashambulio mkesha wa Mwaka Mpya.
“Nina furaha kwamba hakuna chochote kibaya kilichotokea na natumai hali itasalia hivyo,” alisema waziri Joachim Herrmann.
Wapiganaji kati ya watano na saba wanadaiwa kushiriki mpango huo wa kutekeleza mashambulizi, mkuu wa polisi wa Munich Hubertus Andra amesema.
Munich
Image captionPolisi wa Munich walitahadharisha watu kupitia Twitter
Idara ya taifa ya uchunguzi wa jinai Ujerumani ndiyo iliyowapasha habari polisi wa Munich baada ya kupashwa habari na idara nyingine ya ujasusi, Bw Herrmann amesema.
Vyombo vya habari nchini Ujerumani vinasema habari hizo zilitoka kwa idara ya ujasusi ya Ufaransa.
Wasiwasi wa kutokea kwa mashambulio ulikuwa tayari umeifanya miji kadha kufutilia mbali au kuweka masharti kwenye sherehe za kuukaribisha Mwaka Mpya.
Mjini Brussels, maafisa walifutilia mbali sherehe rasmi ya kila mwaka ya kulipua fataki baada ya watu watatu kukamatwa Alhamisi wakihusishwa na njama ya kutekeleza mashambulio mkesha wa Mwaka Mpya.
Watazuiliwa kwa saa 24 zaidi, viongozi wa mashtaka wamesema.
Washukiwa wengine wawili walikamatwa mapema wiki hii.