KOCHA wa timu za soka za taifa za wanawake Rogasian Kaijage amejiuzulu nafasi hiyo.
Kwa muda mrefu Kaijage amekuwa kocha wa timu za wanawake ile ya wakubwa Twiga Stars na ya vijana chini ya umri wa miaka 20 Tanzanite.
Kaijage aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook kwamba imembidi aondoke kwenye nafasi hiyo ili kuamsha ukombozi wa timu hizo.

“Wanangu na wajukuu zangu wa Twiga na Tanzanite, nasikitika saana kuwaacha njiani, lakini imebidi iwe hivyo, sababu mazingira hayanipi mwanya wa kuwasaidia kupata maendeleo niliyoyakusudia”. “Naomba msikate tamaa muongeze bidii Mungu atawasaidia, nami bado nitakuwa nanyi muda wote bora nitafute njia nyingine ya kuweza kuwasaidia nikiwa nje ya timu, kumbuka ilimbidi Yesu afe ili watu wakombolewe hivyo nami imenibidi nitoke ili kuamsha ukombozi wenu,” “Bado nipo nanyi, nawapenda sana,” aliandika Kaijage jioni ya jana.
Baada ya kuandika taarifa hiyo kwenye ukurasa wake mmoja wa makocha wakongwe nchini Kennedy Mwaisabul ‘Mzazi’ aliuliza: “Hatukuelewi kocha”.
Kaijage akajibu: “Mzazi wewe mkongwe nahisi unaweza kuelewa vizuri zaidi matatizo ya mpira kuliko vijana wetu, ukiona mtu mzima analia ujue kuna jambo vijana wanaweza kukurupuka lakini mtu mzima kama mimi niliyepitia matatizo lukuki?”.
“Nakubaliana na wewe asilimia 100 nilikuwa naona mazingira na jitihada binafsi ulizokuwa ukizifanya lakini watu wanataka kwenda peponi bila kufa,” alijibu Mzazi ambapo Kaijage alimjibu “Umenena mzazi”.
Kaijage aliiongoza Twiga Stars kwa karibu miaka mitano baada ya kuchukua mikoba kutoka kwa Charles Mkwasa aliyejiuzulu.
Aliiongoza Twiga kufuzu fainali za Afrika zilizofanyika Congo Brazzavile Septemba mwaka jana.
Mwishoni mwa mwaka juzi akaongezewa kufundisha Tanzanite.
Mara kadhaa Kaijage alikuwa akilalamika kutothaminiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kwamba programu zake alizokuwa akizipangia timu zake zilikuwa zikipuuzwa.
Taarifa ya TFF ilithibitisha kujiuzulu kwa kocha huyo na kusema kwamba TFF itaendelea na programu ya kuendeleza soka ya wanawake pamoja na kwamba utaratibu wa kuteua kocha mwingine atakayeiongoza Twiga katika mechi ya kimataifa dhidi ya Zimbabwe Machi mwaka huu unafanywa.