BODI ya Pamba Tanzania (TCB) imesema inatarajia kufumua mfumo mzima wa ununuzi wa zao hilo nchini unaotajwa ulikuwa ukisababisha baadhi ya wakulima kuharibu ubora wake na kuishusha ubora soko la ndani na la kimataifa.
Mchakato wa kuondoa mfumo huo unatokana na baadhi ya kampuni za kuchambua pamba ambazo zimekuwa zikiwapatia fedha mawakala kwenda kununua pamba kwa wakulima na kuchezea mizani wapate faida.
Kutokana na ‘mchezo’ huo wa kampuni kupunja wakulima kilo zao, kitendo hicho kinadaiwa kuwafanya pia wakulima kuweka maji, mawe na mchanga kuongeza uzito na hatimaye kuharibu zao hilo.

Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba Tanzania, Gabriel Mwaro alisema hayo juzi alipokagua na kukabidhiwa jengo la Maabara ya Pamba mjini Shinyanga.
Jengo hilo lililogharimu Sh milioni 500.5, litatumika kwa shughuli za kupima ubora wa pamba na kuitafutia soko la kimataifa kwa kuinua uchumi wa taifa na mkulima.
Mwaro alisema, kutokana na zao hilo kushuka thamani yake kwenye masoko ya kimataifa kwa sababu ya uchafu na mbegu kuoza, wanatarajia kukaa na kufumua mfumo huo wa ununuzi. Badala yake, wataunda vikundi vya wakulima wa zao hilo na kuwawezesha mashine ndogo za kuchambua Pamba na kuiuza wenyewe viwandani.
“Kabla ya kufumua mfumo huu wa ununuaji pamba tutakaa kwanza na wakulima na kuwapatia elimu hii wakishakubali wataunda vikundi na kuwapatia mkopo wa mashine ndogo za kuchambua pamba ambazo zinauzwa Sh milioni 32, watauza pamba pamoja na mbegu na kupata faida kubwa,” alisema Mwaro.
Alisema, “zoezi hili tukifanikiwa tutakuwa tumekomesha kabisa tatizo la uchafuzi wa zao la pamba hapa nchini na kuirudisha katika ubora wake pamoja na bei kuwa kubwa kwa sababu bei ya pamba huwa inapangwa kwa kutegemea na mahitaji ya soko la kimataifa,” alisema.
Meneja wa Pamba, Kanda ya Ziwa, Buruma Kalindushi alifafanua kuwa mbali na kusambaratisha mfumo huo wa ununuzi, pia watahamasisha mkulima kuingia kwenye Kilimo cha Mkataba. Kilimo hicho kimeelezewa kuwa kitampatia mkulima faida na kuondokana na changamoto tangu hatua za awali mpaka mauzo.