CHANGAMOTO za udini, ukanda, rushwa na kukosekana kwa uhuru wa vyombo vya habari, kumetajwa kulitia doa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Wakizungumza katika kongamano la kutathimini uchaguzi huo lililofanyika katika Ukumbi wa Nkrumah wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam jana, wasomi mbalimbali walionya kuwa kuna kila dalili, suala la udini linashika mizizi katika chaguzi.

Akitoa mada kuhusu namna Uchaguzi Mkuu ulivyoacha salama misingi ya utaifa, mshikamano, usawa na utu katika kongamano hilo, Mhadhiri wa UDSM, Dk Ramadhani Lupa, alisema katika siasa za Tanzania, kumeibuka muingiliano mkubwa wa viongozi wa dini na siasa.
Kwa mujibu wa Dk Lupa, viongozi wa siasa wamebuni mbinu kwa kujua kuwa viongozi wa dini wana kundi la watu nyuma yao, hivyo kukiwa na shughuli za dini wanakwenda kutoa michango mikubwa na baada ya kuchangia shughuli hizo za dini, viongozi hao wa dini huwapa sifa kubwa.
Alitaja matukio yaliyolalamikiwa kuwa ni pamoja na aliyekuwa mgombea wa urais wa Chadema, Edward Lowassa kuonekana akiomba kura kwa kutumia dini, hasa madhehebu ya Walutheri na mgombea wa ubunge wa Isimani, William Lukuvi (CCM), kuonekana akitoa hotuba ya kisiasa kanisani.
Mbali na matukio hayo, Dk Lupa pia alitaja tukio la Shehe mmoja na Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, kuzindua kampeni za Chadema, lakini wakatoa dua mbaya iliyoonekana kama laana.
Matukio mengine aliyoyataja kwamba yaliashiria kuingia kwa udini, Dk Lupa alisema ni pamoja na kundi la watangaza nia karibu 40, waliokuwa wakiwania nafasi ya kuwa mgombea wa urais kupitia CCM, nusu yao kwenda kwa Mchungaji mashuhuri wa Nigeria, TB Joshua.
Kwa mujibu wa Dk Lupa, msafara wa wagombea hao kwa TB Joshua, huenda ulimshitua kiongozi huyo wa dini, ndio maana baada ya kumalizika kwa uchaguzi, alifanya ziara nchini.
Mbali na udini, Dk Lupa alisema pia kuliibuka ubaguzi kwa misingi ya ukanda, hasa Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Ziwa na rushwa, mambo aliyosema yamesababishwa na umasikini, ujinga, ubutu wa sheria na uwiano usio sawa wa kipato kati ya wanasiasa na wataalamu.
Kuhusu vyombo vya habari, mtoa mada Dk Ayubu Rioba kutoka UDSM, alisema akilinganisha miaka iliyopita na mwaka huu, kumekuwa na mabadiliko chanya katika utoaji wa habari, ingawa wagombea waliotangazwa walikuwa Lowassa na aliyekuwa mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli.
Naye mdadisi wa mada hiyo ya vyombo vya habari na demokrasia, Profesa Bernadeta Killian, mbali na kushauri Watanzania wasome kwa undani mada ya Dk Rioba, lakini pia alisema katika baadhi ya maeneo, vyombo vya habari havikuonesha weledi, kama vilivyoonesha katika Uchaguzi Mkuu wa 2010.
Hata hivyo Profesa Killian, alisifu vyombo vya habari kwa kutangaza kampeni za wapinzani katika uchaguzi huo, kiasi cha CCM kuhofia kukosa nafasi ya kutoa habari zake, tofauti na ilivyokuwa huko nyuma ambapo habari nyingi zilikuwa na chama tawala peke yake.
Naye Mwenyekiti wa kongamano hilo, Profesa Issa Shivji, alionya kwamba katika mfumo wa sasa wa ujasiriamali wa kisiasa, ambapo watu wanatumia siasa kupata mali, si rahisi vyombo vya habari binafsi, vinavyoitwa huru kufanya kazi bila upendeleo.
Alifafanua kwamba katika Uchaguzi Mkuu uliopita, baadhi ya vyombo hivyo vinavyomilikiwa na watu binafsi, vilikuwa na upande na mtu akifanya tathimini ya kina, atabaini vilifikia hatua katika hilo, ikawa rahisi hata kujua vichwa vya habari vya magazeti katika siku inayofuata.