WAFANYABIASHARA waliokopeshwa fedha kupitia Mpango Maalumu wa Kuagiza Bidhaa na Malighafi kutoka Nje (CIS) na kukwepa kulipa, sasa ‘wanapumulia mashine’ baada ya serikali kuwabana kulipa madeni yao ndani ya miezi sita kuanzia jana.
Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Servacius Likwelile, alisisitiza kwamba wadaiwa watakaoshindwa kulipa madeni yao katika kipindi hicho, watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo majina yao kutangazwa kwenye vyombo vya habari umma uwatambue.
Ili kudhihirisha kusudio lake la kuhakikisha kuwa wadaiwa wanalipa fedha hizo, Dk Likwelile alisema awamu hii, serikali imeingia Mkataba na Kampuni ya Kufuatilia Madeni ya Msolopa Investment ya jijini Dar es Salaam kuwafuatilia wadaiwa wote na kuhakikisha wanalipa ndani ya kipindi hicho.
Dk Likwelile alisema katika juhudi hizo mpya wadaiwa waliokuwa wanafuatiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wanapaswa kuwasiliana na mamlaka hiyo waweze kupata kumbukumbu za madeni yao, vivyo hivyo kwa wadaiwa waliopata mikopo yao kupitia Benki ya Rasilimali (TIB), kuwasiliana na benki hiyo kwa madhumuni kama hayo.
Alipotafutwa na gazeti hili, mmoja wa maofisa wa Kampuni ya Msolopa Investment ambaye hata hivyo aliomba jina lake kutotajwa kwa madai kuwa si msemaji kwa suala hilo, alidokeza kwamba hatua za awali za kuwasiliana na wadaiwa wa fedha hizo za CIS zimeshaanza kuchukuliwa.
“Ninachoweza kudokeza kwa kifupi ni kwamba tumeanza kuwaandikia barua wadaiwa wote kwa mujibu wa orodha tuliyokabidhiwa na Wizara ya Fedha na Mipango. Kwa sasa hatuwezi kusema lolote hadi pale tutakapokamilisha mchakato wa awali.
“Lakini kama ulivyosikia baada ya miezi sita kama wahusika wasipolipa watachukuliwa hatua kali, ikiwa ni pamoja na majina yao kutangazwa kwenye vyombo vya habari,” alisema ofisa huyo.
Mbali ya kauli ya Dk Likwelile jana, juzi Serikali ilitoa matangazo kupitia magazeti mbalimbali likiwemo gazeti hili, ikiwaamuru wadaiwa hao iliowaita sugu wa fedha za CIS kujitokeza na kulipa madeni hayo ndani ya miezi sita ijayo.
Chimbuko la CIS Kuanzia miaka 1980 mpaka 1992/1993, wahisani mbalimbali walitoa fedha za kigeni kwa mpango huo wa CIS kwa lengo la kuipa serikali uwezo wa kuimarisha uchumi wake kwa kuzipatia taasisi, kampuni, viwanda na biashara mbalimbali uwezo wa kuagiza bidhaa na malighafi kutoka nje kwa kuwa wakati huo nchi ilikuwa na upungufu mkubwa wa fedha za kigeni.
Fedha za CIS zilitolewa kama mikopo yenye masharti nafuu, ambapo wakopaji walitakiwa kulipa deni bila kutozwa riba, lakini mkopaji akichelewa kulipa katika kipindi cha miezi 18, mkopo huo huwa na riba ya asilimia 17.
Fedha zilizokusanywa kutokana na malipo ya deni zilikuwa zinachangia mapato ya serikali (bajeti) pamoja na miradi maalumu ya maendeleo baada ya makubaliano na wahisani husika.
Zaidi ya kampuni 980 zilikopeshwa fedha chini ya utaratibu huo, lakini pamoja na jitihada kubwa za serikali, urejeshaji wa mikopo hiyo umekuwa si wa kuridhisha, kwani bado wadaiwa wengi hawaoneshi nia ya kurejesha mikopo hiyo.
Chini ya mpango huo, serikali iliwakopesha wafanyabiashara fedha za kigeni kwa ajili ya kulipia bidhaa zao na baadaye kuwataka warejeshe kwa Shillingi ya Tanzania kupitia Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), lengo likiwa ni kuwasaidia wafanyabiashara wasikwamishwe katika uagizaji wa bidhaa kutoka nje.
Hata hivyo pamoja na ukweli kwamba wafanyabiashara waliwezeshwa kupunguza madeni yao bado serikali ilibakia na mzigo wa madeni kwa wafadhili walioikopesha chini ya mpango huo wa CIS.
Hivyo sambamba na mpango wa CIS na EPA ilibidi serikali ibuni mkakati au mpango mwingine wa kulipa madeni yake ya nje. Ndipo ulipobuniwa Mpango wa Debt Conversion (DCP).
|
0 Comments