WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ndiyo kitovu cha nchi na kwamba kila Mtanzania ameelekeza jicho lake pale kwa sababu anasubiri kupata huduma ya msingi.
“Hapa ndipo kitovu cha nchi na Watanzania wote macho yao yako huku. Kwa nini? Kwa sababu huduma zinazowagusa za barabara, maji, elimu, zinatokea huku kwa maana ya bajeti na usimamizi,” alisema.
Alitoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza na wakurugenzi, wakuu wa taasisi na watumishi wa Ofisi ya Rais – Tamisemi kwenye mkutano uliofanyika ofisi ya Tamisemi mjini Dodoma.
“Wananchi wakilalamikia ukosefu wa hizi huduma chanzo ni hapa. Katika wizara kuna mawaziri lakini wao kule ni wasimamizi wakuu. Ninyi chini yenu kuna mikoa, wilaya, halmashauri, rasimali watu na rasilimali fedha za kuwasaidia kufikisha huduma tarajiwa kwa Watanzania walio wengi,” alisisitiza.
Waziri Mkuu ameitaka ofisi hiyo ihakikishe inaisimamia vizuri mikoa na halmashauri ili Serikali iweze kupata matokeo mazuri na tarajiwa na kuongeza kuwa jukumu kubwa lililopo hivi sasa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ni kuhakikisha kuwa zinabuni vyanzo vipya vya mapato na kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato ya serikali.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano imekusudia kuwahudumia ipasavyo Watanzania wenye uelewa tofauti na matakwa tofauti na kwa kuanzia Serikali imeanza kuwajenga watumishi wa Serikali kutambua kuwa wao ni wahudumu wa wananchi hivyo inawapasa kuwahudumia vema.
Mapema akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na watumishi hao, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tamisemi, George Simbachawene alisema Tamisemi ipo tayari kubadilika na kufanya kazi kama kauli ya Rais John Magufuli inayosema Hapa Kazi Tu.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bernard Makali alimpongeza Waziri Mkuu Majaliwa kwa kusimamia vizuri masuala ya elimu nchini wakati akiwa Naibu Waziri wa Tamisemi anayeshughulikia masuala ya elimu.
0 Comments